Pages

Saturday, January 13, 2018

Tishio la usalama wa vifaa vya kompyuta: Inamhusu kila mtumiaji wa desktop, laptop, tablets, smartphone, na vingine.

Utangulizi
Takribani siku kumi zilizopita, wataalamu bingwa wa usalama wa kompyuta walichapisha utatifi ulionesha tatizo kubwa la kiusalama linalozikabili karibu aina zote za vidubwasha vya kompyuta duniani (desktops, laptops, tables, smartphones, and some servers) ambalo halikuwahi kujulikana kabla. Ukubwa wa tatizo hili ni ukweli kwamba linahusika hasa na uwezekano ulio dhahiri wa kompyuta yoyote unayotumia kuweza kudukuliwa taarifa za siri kama nywila (passwords), emails na documents. Utafiti huu (umepewa jina la Meltdown and Spectre Vulnerabilities) ni wa ngazi ya juu katika uhandisi wa kompyuta na nimekosa lugha nyepesi ya kuelezea hasa kwa wasio na utaalamu husika. Hata hivyo, kutokana na umuhim na uzito wake, na kwa kuwa hadi sasa sijasoma popote ulipoelezewa kwa lugha nyepesi katika vyombo vya habari na mitandao ya hapa nchini, ngoja nijaribu kufanya hivyo kwa manufaa ya watakaosoma.

Meltdown and Spectre Vulnerabilities: Source here
Nini cha kuelewa kwanza kuhusu kifaa chako?
1.    Kifaa chochote cha kielekroniki kinakamilika kuwa kompyuta kwa vitu vikubwa vinne: (1) Hardware (yaani kasha la nje na sehemu zingine za ndani ya kompyuta. Huu ni mwili wa kompyuta ambao bila kuwa na uhai ndani yake ni mfu na hauna kazi); (2) Operating system (Hii ni nafsi hai au uhai wa kompyuta – ambao lazima uwe ndani ya mwili (hardware) ili uonekane na kuufanya mwili kuwa na matumizi); (3) Application software (yaani maarifa au ujuzi (skills) unazoiwezesha kompyuta hai kufanya kazi  mbalimbali na mahususi); na (4) Processor (hii ni moja ya ya hardware ambayo ndio yenye intelligence au ndio ubongo wa kuratibu kila kinachoendelea kwenye kompyuta - bila processor kompyuta ni inakua zaidi ya zezeta/ jinga/ zombie/ nk kwani haitakua na uwezo wa kuwa hai).

2.    Hakuna kidubwasha chochote cha kompyuta unachotumia kisichotegemea processor (au microprocessor). Hadi sasa kuna aina kubwa tatu za microprocessors zinazotumika na vifaa vingi na kutegemea aina ya kompyuta unayotumia. Nazo ni Integrated and electronics (Intel) microprocessor; Advanced Micro Devices (AMD) microprocessor na Advanced RISC Machine (ARM) microprocessors.

3.  Kwa kompyuta kubwa kama servers zinazohitaji processing power kubwa zaidi, zinatumia aina nyingine ya processors hasa za International Business Machines (IBM) cooperation zijulikanazo kama "POWER series high performance microprocessors".

4.  Kama nilivyosema awali, processors ni hardware na sio software. Hata hivyo inafanya kazi zake kwa kutumia software maalumu. Hivyo bila kujali kompyuta yako inatumia operating system gani (Apple/Mac, windows, android, Linux, nk), inaweza kuwa inatumia aina mojawapo ya processors yoyote kati ya nilizotaja kulingana na chaguo la mtengezaji wa kifaa husika. Hadi sasa vidubwasha vingi vinatumia Intel kutokana na ubora na sababu zingine za kiuchumi na kibiashara (competitive advantage).
Intel Microprocessor : source here
Tatizo liko wapi?
Kile tunachokifurahia kwa kuwa na vifaa/vidubwasha vya kielekroniki vyenye uwezo mkubwa wa kufanya vitu vingi kama simu za mikononi, laptops na vingine, inatokana na ubunifu wa wahandisi wa microprocessors. Hata hivyo ubunifu huo unatumika kwa gharama kwani umepelekea tatizo la kiusalama. Kwa nini? Kuna mambo mawili:

Friday, September 15, 2017

Miujiza ya CASSINI: Chombo cha utafiti wa anga la mbali kilichovunja rekodi ya mafanikio

[​IMG]
CASSINI ikiwa kati ya Saturn mwezi wa Titan amboa ni mkubwa zaid kati ya miezi 60 inayozunguka Saturn

Utangulizi

Leo ni siku ya kihistoria na mafaniko makubwa kwa wanasayansi wa elimu ya anga duniani (astronomers) kwani majira ya saa tisa mchana kwa saa za Tanzania chombo kilichokaa angani kwa miaka 20 kikifanya utafiti kilifikia mwisho wa uhai na kazi yake. Tarehe 15 Octoba mwaka 1997 (miaka 20 iliyopita), wanasayansi walituma chombo cha anga (spacecraft) kilichoitwa CASSINI HUYGENS kwenda kwenye anga la sayari ya Saturn kufanya utafiti. Safari hii (Space Mission) iliandaliwa kwa ushirikiano wa kituo cha anga cha Marekani (National Aeronautics and Space Administration - NASA) wakishirikiana na taasisi ya anga ya Ulaya (European Space Agency - ESA) na kile cha Italia Space Agency (ASI). Chombo hiki kilikua ni jaribio la nne ya kutuma vyombo vya kitafiti katika sayari hii na ni hiki pekee ambacho kilifanikiwa kuingia katika anga la Saturn na kuzunguka katika orbit yake zadi ya mara 20 kikikusanya taarifa.


Tuesday, July 25, 2017

Wanafunzi wanaoomba kujiunga na vyuo vikuu: Je, ukasome shahada na chuo gani?

Vyuo vikuu vya Tanzania vimefungua madirisha ya usajili mpya kwa ajili ya muhula wa masomo wa mwaka 2017/2018. Sio vyuo vya Tanzania tu bali karibu nchi nyingi huu ndio muhua wa kudahili wanafunzi wapya. Hiki ni kipindi muhum sana kwa vijana wetu hasa wanaoanza shahada ya kwanza kwani ile ndoto yao ya kupata “DEGREE” na kuwa “MSOMI” ndio inaanza kuwa na ukweli. Hivyo ni muhim sana vijana hawa wakapata mwangaza wa kutosha wanapochagua chuo gani cha kujiunga na kwa ajili ya kusoma programme gani.

upload_2017-7-25_11-57-24.png 

Wale walio kwenye vyuo vikuu wanaelewa changamoto ambazo huwa tunakutana nazo kama waalimu/wahadhiri nyakati kama hizi. Wanafunzi wengi hawajui wakasome programme gani na kwa nini. Hili tatizo sio dogo kwani mara nyingine tunafundisha wanafunzi madarasani ambao hawajui walichochagua kusoma kinawapeleka wapi. Wengi hawajui nini iwe msingi wa maamuzi ya chuo gani cha kusoma. Mbaya zaidi, mara nyingi vijana hawa wanashauriana wao kwa wao au kushauriwa na watu wasio na uelewa wa mambo ya kitaalamu kwa taarifa zisizokua sahihi, zisizokua na ukweli, na za kupotoshana. Wako vijana wengi wamefeli chuo kikuu sio kwa sababu hawana uwezo bali kwa kuwa walijipachika kusoma vitu ambavyo havimo ndani yao bali walijiunga kwa mkombo, kutokujua au kushauriwa vibaya.

Monday, May 15, 2017

Uvamizi wa Udukuzi wa Kompyuta Umekuja Kivingine: ni Hatari Kuliko Juzi Tuchukue Hatua Haraka

europol.jpg

Ninaandika mara ya tatu mfululizo kuhusu Udukuzi wa Mifumo ya Kompyuta ulioikumba dunia siku ya nne sasa (Global Cyberattack) kutokana na uzito wa tatizo hili na uhatari wake kwa usalama wetu. Nina ufahamu mpana wa matumizi ya mifumo ya kompyuta kwenye nchi yetu hivyo ninaelewa udhaifu (weak points) unaoweza kutugharimu na kutuacha pabaya. Na hili ndilo linanifanya nitumie muda huu adimu kuendelea kuelimisha, kutoa taadhari na kushauri nini cha kufanya. Msingi wa tatizo hili uko kwenye makala niliyoandika Jumamosi (HII HAPA).

Kama nilivyoandika kwenye makala ya jana Jumalipi (HII HAPA) kwamba, pamoja na mafanikio makubwa ya kijana mmoja nchini Uingereza siku ya Jumamosi kuzuia kusambaa kwa kirusi WannaCry, bado haukua mwisho wa tatizo. Athari kubwa ya udukuzi huu inategemewa kuonekana leo Jumatatu watu wataporudi makazini na kuwasha kompyuta zao. Lakini pia nilisema kwamba wataalamu wamejiweka mguu sawa kupambana na shambulio kubwa zaidi kuliko la Ijumaa kwa sababu hii biashara ya udukuzi wa Ransomware inalipa sana na hawa jamaa ni lazima watafute njia nyingine ya kushambulia. Na wangefanya hivyo baada ya kubadilisha design (coding) ya programu ya kirusi WannaCry. Hiki ndicho kimetokea.

Sunday, May 14, 2017

Kirusi Dukuzi Kimedhibitiwa Kusambaa ila Tatizo Halijaisha: Ushauri Jumatatu Makazini

Wannacry.PNG 

Tanzania imekua miongoni mwa nchi za kwanza kabisa katika bara la Afrika kushambuliwa na udukuzi wa kimtandao uliosambaa kwa kasi siku ya Ijumaa kwenye nchi 99 duniani. Baada ya wataalamu wa usalama wa mifumo ya kompyuta kupitia wakati mgumu wa mwisho wa wiki, hatimaye kijana mdogo wa miaka 22 nchini Uingereza amefanikiwa kudhibiti kusambaa kwa kirusi 
WannaCrypt aliyeitingisha dunia. Kijana huyu anayejitambulisha kwa jina kama Malware Tech (hatumii jina halisi kwa sababu za kiusalama wa kazi yake) ni mtafiti wa uchambuzi wa virusi vinavyoshambulia mifumo ya kompyuta (Malware Analysist)alifanikiwa kazi hii baada ya kazi ya zaidi ya masaa 24 aliyoianza jana Ijumaa saa nane mchana. Jioni ya Jumamosi ameelezea vema katika blog yake ya Malware Tech kazi aliyoifanya hadi kufanikiwa kuzuia kirusi huyu kusambaa.

Pamoja na habari njema hii ni vema tukawa na ufahamu wa kutosha juu wa kilichotokea na kujua tunatakiwa kufanya nini. Nitaandika mambo machache.

Kwanza fahamu yafuatayo:

Saturday, May 13, 2017

Uvamizi Hatari wa Kimtandao Duniani: Tishio la Usalama wa Taifa Tuchukue Hatua Haraka

Jana usiku nimetoa taadhari kwenye moja ya taasisi za umma juu ya Global Cyberattack - uvamizi wa kutisha wa udukuzi wa mifumo ya kompyuta - uliotokea kwa muda kidogo na kushika kasi ya ajabu siku ya jana - nikiwataka wachukue hatua za haraka kujilinda.

Hata hivyo nimeona niweke maelezo na ushauri wangu kwenye public maana jambo hili ni utishio kubwa kwa usalama wa taifa na hadi ninapoandika makala haya, udukuzi huu unaendelea kusumbua mifumo ya computer duniani kote.

Leo hii nimepata taarifa za uhakika juu ya taasisi, makampuni na watu binafsi ambao wameshathirika na udukuzi hata kwetu Tanzania.

Kwa kifupi huu ni udukuzi wa kimtandao ambao umeathiri nchi takribani 100 duniani kwa siku ya jana tu. Nchi zenye wataalamu wa hali ya juu, mifumo ya kisasa, na uwezo mkubwa wa ulinzi na udukuzi wa mitandao kama Uingereza, Urusi, Ujerumani, na Ukrain wameathiriwa sana. Kama hawa yamewakuta ni wazi kwamba sisi tuko kwenye hatari kubwa na tunalazimika kuchukua hatua za haraka kama nchi na kama mtu mmoja mmoja.

20170512_230726.jpg


Pamoja na kwamba hakuna taarifa/reports nyingi kutoka Tanzania na Afrika kwa ujumla juu ya uvamizi huu, ukweli ni kwamba nchi za kiafrika zimeshavamiwa tangu jana. Uhalifu huu mpya wa udukuzi unaendeshwa na majangili wenye utalaamu mkubwa wa mitandao na wamejificha nyuma ya pazia la chuma lisilopenyeka kirahisi.

Thursday, May 11, 2017

Unywaji wa kahawa unaweza kukukinga na magonjwa ya moyo

UTANGULIZI: Makala hii fupi ya kisayansi tuliandika mwakaa 2015 na kuomba kuichapisha kwenye magazeti kadhaa ya Tanzania kwa kuwa tulijua sio watu wengi watakaoweza kuusoma huo utafiti na kufaidi yaliyomo. Pia tuliona utafiti huu ni chachu kwa nchi yetu hasa kutokana na ukweli kwamba kahawa ni moja ya mazao muhim ya biashara nchini.

Hata hivyo magazeti yote tuliyoomba walitukatalia maana hawakua na interest nayo na wengine hawakutujibu kabisa (Ni ngumu sana kupata nafasi ya kuandika makala kwenye magazeti yetu hasa kama hakuna mtu anayekufahamu kwenye chombo husika).

Baada ya kukwama tuliamua kuiweka kwenye blog ya www.wavuti.com. Lakini kwa umuhim na uzito wa utafiti huu wa Bwana Choi na wenzake, nimeona ni vema niweke tena hapa andiko hili ili kuwapa nafasi wanaotembelea kurasa hizi maarifa ya kuwasaidia na wawashirikishe wengine. Karibu ujisomee.


Khawa.jpgUtafiti uliofanywa nchini Korea na mtafiti Choi na wenzake na kuchapishwa mwezi Machi kwenye jarida la kisayansi liitwalo Heart, umechangia sana kuondoa utata uliokuwepo kwa muda mrefu kuhusu ubora au madhara ya kiafya yatokanayo na unywaji kahawa. Utafiti huo ambao ni mkubwa sana ulihusisha zaidi ya watu elfu ishirini na tano (25,000) umeonesha unywaji wa kahawa hadi vikombe 5 kwa siku husaidia kupunguza maradhi ya moyo.

Wednesday, March 1, 2017

Matumizi ya simu wakati wa kuendesha gari: moja ya tishio jipya la maisha duniani

Siku za karibuni tumeona hatua ya jeshi la polisi kutumia ushahidi wa picha na video za mitandaoni katika kufuatilia makosa ya madeva barabarani. Jambo hili ni la kupongezwa sana na kuunga mkono. Watu wengi hupenda kupiga picha za kujidai wakiwa wanaendesha magari huku wakiwa hawajafunga mikanda, wanatumia simu kujirekodi, nk, na haya sio mambo ya kuvumilia kwa nchi inayotaka kufuata sheria na taratibu zilizowekwa. Ningetamani kitengo cha mitandaoni cha jeshi la polisi kichukue hili kama moja ya jukumu la ufuatiliaji na wasiishie kwa wale tu ambao wamejulikana kama Diamond. Nataka nizungumzie moja ya makosa haya na nitatoa mfano wan nchi moja ambayo kwa sehemu kubwa tumerithi mfumo na sheria zao
Dai1.jpg 
Ajali za barabarani zinazotokana na matumizi ya simu za mikononi wakati wa kuendesha gari zimeongezeka sana duniani kote na zinagharimu maisha ya watu wengi sana na kuacha wengi wakiwa vilema na upotemvu mkubwa wa mali. Nchi nyingi duniani zinabuni hatua mbalimbali za kupunguza tatizo hili. Pamoja na elimu kubwa kwa raia, matangazo barabarani, na mafunzo mbalimbali, wanaweka sheria ngumu ili kupunguza uwezekano wa madereva kufanya makosa. Sina hakika iwapo nchi yetu tuna rekodi sahihi za ajali zinazohusianishwa na utumiaji wa simu hasa kutokana na ukweli kwamba hatuna mifumo mizuri ya kutunza taarifa, kuchunguza, na kuthibitisha vyanzo vya ajali kwa vielelezo. Pia kuna shuhuda nyingi ya sababu za ajali kuandikwa kinyume na chanzo halisi kwa sababu ambazo nisingependa kuzitaja hapa. Ila iwavyo vyovyote vile, kuna ajali nyingi sana zinasababishwa na matumizi ya simu kwa madereva. Jambo hili linahitaji kuchukuliwa kama janga na kupewa uzito wa kutosha tukianzia na elimu kwa jamii kukubali kubadilika na kuacha kuwa watumwa wa mawasiliano hata pale isivyo lazima. Ni lazima kila anayeendesha gari ajishawishi kutotumia simu na raia wawe wakali wanapoona dereva anafanya hivyo. Tafiti nyingi zilizofanyika nchi nyingi duniani zimeonesha kwamba matumizi ya simu wakati wa kuendesha gari yanamwondoa dereva katika umakini (concentration) ya kinachoendelea barabarani na hivyo kumweka katika hatari kubwa ya kufanya makosa au kushindwa kuchukua hatua kwa wakati pale inapojitokeza hatari.

Saturday, January 14, 2017

NI NJIA GANI ITAYOKAYOKUHAKIKISHIA USALAMA NA USIRI WAKO WAKATI WA MAWASILIANO?

Utangulizi:
Usiri (confidentiality) na usalama (security) ni dhana na bidhaa mbili zenye umuhim mkubwa sana kwenye mawasiliano kwa njia za kielekroniki kama simu, ujumbe mfupi wa maandishi, na baruapepe (emails). Moja, ni uhakika kwamba nikiongea na mtu kwa simu au kwa ujumbe wa maandishi (SMS au programu zingine zinazoruhusu kuchati) au kwa baruapepe (emails) hakuna mtu mwingine asiyehusika ambaye anaweza kuyasikia au kuyaona mawasiliano yangu (confidentiality). Mbili, ni uhakika kwamba ninapofanya mawasiliano, mtu au watu wenye lengo la kufuatilia mawasiliano yangu hawataweza kufanya hivyo kwa kuwa nina ulinzi dhidi ya kuingiliwa (kusikiliza sauti au kuona ujumbe) mawasiliano yangu (Security). Haya mambo mawili ni mahitaji makubwa kwa mteja yeyote wa huduma ya mawasiliano duniani kote.

Jinsi mawasiliano ya simu yanavyoweza kuingiliwa.  Chanzo: mtandao wa Internet 

Sio lengo la makala hii fupi kukuchosha kwa kuongea kwa undani utaalamu na teknolojia za mawasiliano na jinsi zinavyofanya kazi bali nataka tu kumishirikisha elimu kidogo kwa wale wasio na uelewa wa kutosha na hivyo kumisaidia mambo kadhaa: moja, kujua njia sahihi ya kutumia kulingana na aina ya mawasiliano; mbili, kujua njia gani sio sahihi kuwasiliana wakati gani; tatu, kujua jinsi ya kujilinda na kujihakikisha usalama na usiri kwenye mawasilinao; na nne, kuwa na ujasiri au kujiamini unapowasiliana kwamba uko salama. Hali kadhalika, inaweza kumisidia baadhi ya watu kujua ni aina gani ya simu au vifaa vingine wanavyohitaji kulingana na asili ya mawasiliano yao. Hata hivyo, makala hii haina lengo la kumshawishi au kumsaidia mtu kufanya uhalifu na kuvunja sheria zihusianazo na makosa ya mawasilinao ya kimtandao.

Monday, January 4, 2016

MADHARA YA SIMU ZA MIKONONI KATIKA MAHUSIANO YA KIJAMII? SEHEMU YA PILI

Kwa nini simu za mikononi ni tishio kwa jamii yetu?
Katika makala hii na zitakazofuata, ninapotumia neno matumizi ya simu za mkononi, ninamaanisha mawasiliano ya kupiga na kupokea simu; utumaji na upokeaji wa ujumbe mfupi wa simu (SMS); matumizi ya mitandao ya kijamii kupitia simu; kucheza games kupitia simu; kutuma na kupokea barua pepe; na matumizi mengine ya intaneti kupitia simu.

Tangu kugunduliwa kwa teknolojia ya simu za mikononi, imekua na kuenea/kusambaa kwa haraka sana duniani kuliko teknolojia nyingine yoyote ile ambayo imewahi kugunduliwa katika historia ya mwanadamu. Kwa mfano: wakati ugunduzi wa runinga umetokea miaka kama 100 iliyopita, Tanzania bara tumeanza kutazama runinga kama miaka 25 tu iliyopita. Kulingana ya repoti ya mwisho wa mwaka 2014 ya Mamalaka ya Mawasiliano nchini (TCRA), Tanzania nzima kuna wastani wa runinga 1,000,000 pekee. Simu za mezani (landline au za TTCL) zimegunduliwa kwa mara ya kwanza na mskotishi Alexander Graham Bell mwaka 1876 lakini hadi mwezi wa tisa mwaka huu ni wateja (subscribers) takribani 304,000 pekee ndio wanamiliki simu hizi. Hali kadhalika, wakati ugunduzi wa internet umetokea miaka ya 1960, Tanzania tumeanza kutumia internet mwishoni mwa miaka 1990 tena kwa watu wachache sana. Hadi mwezi wa tisa mwaka 2015 ni takribani watu 1.9M pekee ndio wanamiliki (subscribers) huduma hii ikiwa ni pamoja na maofisi. Mashine za kufulia nguo (washing machines) zimeanza kutumika nchini Sweden mwanzoni mwa miaka ya 1950 lakini hadi sasa watanzania wanaotumia teknolojia hii kama kifaa cha nyumbani ni wa kutafuta na huenda kuna mikoa haina hata mashine moja. Usambazaji umeme umefanyika kwa mara ya kwanza nchini Uingereza mwaka 1881 lakini hadi leo miaka 135 baadaye, umeme ni huduma ya anasa Tanzania na umewafikia watu chini ya 40%.