Pages

Saturday, November 21, 2015

"Hotuba ya Rais JPM ya Kufungua Bunge la 11, Inanishawishi kwamba alisoma Makala yangu"

Nimemsikiliza Rais Dr. John Pombe Magufuli alipokua anatoa hotuba ya ufunguzi wa bunge la 11. Hotuba yake (HII HAPA) inaonekana imewajengea watanzania wengi tumaini jipya. Kwa wachache nliowasiliana nao wanajisikia fahari ya utanzania wao baada ya kumsikiliza rais wao. Rais amegusia mambo ya msingi sana yalihusuyo taifa letu na kuonesha ni kwa jinsi gani anazitambua shida na kero za watanzania na kajiandaa kukabiliana nazo kwa nguvu zake zote. Hotuba hii imenikumbusha mambo ambayo niliwahi kuyapendekeza kabla ya kuanza michakatop ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.


Picha kwa hisani ya blog ya Haki Ngowi
Miezi kama mitano iliyopita, niliandika makala kuhusu uchaguzi mkuu wa Uingereza wa mwaka 2015. Katika sehemu ya mwisho ya mfululizo wa makala hiyo niligusia mambo ambayo watanzania wanaweza kujifunza kutokana na uchaguzi huo hasa kwenye dhana ya kuchagua viongozi kwa kigezo cha kutatua changamoto za wananchi. Katika makala hiyo, nilieleza mambo 12 ambayo Rais wa awamu ya tano anatakiwa kuyajua na kuyafanyia kazi ili kuondoa maumivu na mateso ambayo watanzania wamekua nayo kwa muda. Ninaomba niweke sehemu ya makala hiyo niliyoelezea mambo hayo kwani kwa sehemu kubwa Rais ameyaongelea katika hotuba yake ya ufunguzi wa bunge kwa undani na uzito wa kipekee kama nilivyokua nimeandika.
Katika makala hiyo nilionesha ni kwa jinsi gani kampeni za wenzetu zilijikita katika mambo ya msingi ya maisha ya watu wao. Mambo hayo hayakua mapya wala hazikua ahadi za kupeleka watu mwezini: hapana. Hoja zao zilikua zinaakisi mambo halisi za maisha ya  ya kila siku na zilitokana na kauli na kilio cha wananchi bila kujali uzito wala wepesi wake. Masuala yote yahusuyo uhamiaji, kodi, elimu, afya, ulinzi, ajira, uchumi, na mengine yalitamkwa katika uhalisia wake tena kwa undani na kwa data zinazoonesha hali iliyoko na kinachoahidiwa. Kwa kifupi, hoja za kampeni zilikua ni uhalisia wa maisha ya watu na sio ndoto na ahadi za kisiasa zenye lengo ya kununua kura kwa udanganyifu. Sehemu ya makala hiyo ni kama nilivyoiweka hapa chini:

.................
Watanzania tuna mambo yetu ya msingi ambayo yanatusumbua na twahitaji wanasiasa waje na hoja na mipango yao ya nini wanataka kutufanyia watakapokuwa viongozi. Tunataka watu wanaojua matatizo yetu maana wametusikiliza, wanatuelewa, ni wa kweli kwetu, na wanatuheshimu kwamba ndio tuna mamlaka wanayoyatafuta. Baada ya hapo watuambie wanapambanaje na kilio chetu. Hatutaki wanasiasa wanaojifanya wao ni miungu, wanajimu, waganga wa kienyeji au wao ni mti wa mwarubaini kwamba wana tiba ya kila tatizo: hapana. Tunataka watu waliotusikiliza sisi na kubeba hoja zetu kwa uzito uleule tulionao. Kisha wanaposimama kutuomba kura watuambie wanakwenda kuzishughulikia vipi na watupe vigezo vya kuwahukumu iwapo watashindwa kutekeleza wanachoahidi.
Pamoja na kwamba kipenga cha uchaguzi mkuu bado hakijapulizwa na vyama vya siasa bado VIMEGOMA kututajia mapema majina ya watakaogombea nafasi mbalimbali ili kutupa muda wa kutosha kuwahoji na kuwachambua, hoja za msingi juu ya uchaguzi mkuu zinajulikana. Wananchi tunajua ni nini kinatusumbua au tungetamani kifanyiwe kazi na wanasiasa. Tumekua tukilizwa kwa muda mrefu na maumivu makali tunayokutana nayo kwenye maisha ya kila siku na jinsi yanavyotukatisha tamaa na kutuondolea furaha. Ngoja nitaje machache yanayotuumiza vichwa: