Pages

Saturday, November 21, 2015

"Hotuba ya Rais JPM ya Kufungua Bunge la 11, Inanishawishi kwamba alisoma Makala yangu"

Nimemsikiliza Rais Dr. John Pombe Magufuli alipokua anatoa hotuba ya ufunguzi wa bunge la 11. Hotuba yake (HII HAPA) inaonekana imewajengea watanzania wengi tumaini jipya. Kwa wachache nliowasiliana nao wanajisikia fahari ya utanzania wao baada ya kumsikiliza rais wao. Rais amegusia mambo ya msingi sana yalihusuyo taifa letu na kuonesha ni kwa jinsi gani anazitambua shida na kero za watanzania na kajiandaa kukabiliana nazo kwa nguvu zake zote. Hotuba hii imenikumbusha mambo ambayo niliwahi kuyapendekeza kabla ya kuanza michakatop ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.


Picha kwa hisani ya blog ya Haki Ngowi
Miezi kama mitano iliyopita, niliandika makala kuhusu uchaguzi mkuu wa Uingereza wa mwaka 2015. Katika sehemu ya mwisho ya mfululizo wa makala hiyo niligusia mambo ambayo watanzania wanaweza kujifunza kutokana na uchaguzi huo hasa kwenye dhana ya kuchagua viongozi kwa kigezo cha kutatua changamoto za wananchi. Katika makala hiyo, nilieleza mambo 12 ambayo Rais wa awamu ya tano anatakiwa kuyajua na kuyafanyia kazi ili kuondoa maumivu na mateso ambayo watanzania wamekua nayo kwa muda. Ninaomba niweke sehemu ya makala hiyo niliyoelezea mambo hayo kwani kwa sehemu kubwa Rais ameyaongelea katika hotuba yake ya ufunguzi wa bunge kwa undani na uzito wa kipekee kama nilivyokua nimeandika.
Katika makala hiyo nilionesha ni kwa jinsi gani kampeni za wenzetu zilijikita katika mambo ya msingi ya maisha ya watu wao. Mambo hayo hayakua mapya wala hazikua ahadi za kupeleka watu mwezini: hapana. Hoja zao zilikua zinaakisi mambo halisi za maisha ya  ya kila siku na zilitokana na kauli na kilio cha wananchi bila kujali uzito wala wepesi wake. Masuala yote yahusuyo uhamiaji, kodi, elimu, afya, ulinzi, ajira, uchumi, na mengine yalitamkwa katika uhalisia wake tena kwa undani na kwa data zinazoonesha hali iliyoko na kinachoahidiwa. Kwa kifupi, hoja za kampeni zilikua ni uhalisia wa maisha ya watu na sio ndoto na ahadi za kisiasa zenye lengo ya kununua kura kwa udanganyifu. Sehemu ya makala hiyo ni kama nilivyoiweka hapa chini:

.................
Watanzania tuna mambo yetu ya msingi ambayo yanatusumbua na twahitaji wanasiasa waje na hoja na mipango yao ya nini wanataka kutufanyia watakapokuwa viongozi. Tunataka watu wanaojua matatizo yetu maana wametusikiliza, wanatuelewa, ni wa kweli kwetu, na wanatuheshimu kwamba ndio tuna mamlaka wanayoyatafuta. Baada ya hapo watuambie wanapambanaje na kilio chetu. Hatutaki wanasiasa wanaojifanya wao ni miungu, wanajimu, waganga wa kienyeji au wao ni mti wa mwarubaini kwamba wana tiba ya kila tatizo: hapana. Tunataka watu waliotusikiliza sisi na kubeba hoja zetu kwa uzito uleule tulionao. Kisha wanaposimama kutuomba kura watuambie wanakwenda kuzishughulikia vipi na watupe vigezo vya kuwahukumu iwapo watashindwa kutekeleza wanachoahidi.
Pamoja na kwamba kipenga cha uchaguzi mkuu bado hakijapulizwa na vyama vya siasa bado VIMEGOMA kututajia mapema majina ya watakaogombea nafasi mbalimbali ili kutupa muda wa kutosha kuwahoji na kuwachambua, hoja za msingi juu ya uchaguzi mkuu zinajulikana. Wananchi tunajua ni nini kinatusumbua au tungetamani kifanyiwe kazi na wanasiasa. Tumekua tukilizwa kwa muda mrefu na maumivu makali tunayokutana nayo kwenye maisha ya kila siku na jinsi yanavyotukatisha tamaa na kutuondolea furaha. Ngoja nitaje machache yanayotuumiza vichwa:


1- Utaifa na Taifa letu. Moja ya mambo yanayoisumbua nchi yetu kwa miaka ya karibuni ni umoja wa taifa letu na wananchi yake. Kumekua na malumbano na kauli nyingi ambazo kwa namna moja au nyingine zinatishia uhai wa utaifa na umoja wetu uliojengeka kwa miaka mingi. Jambo hili linaweza kuonekana katika maeneo matatu: moja ni swala muungano kati ya Zanzabar na Tanganyika; mbili ni mgwanyiko unajitokeza kikanda au kimikoa: upemba na uunguja, umwanza na ukilimanjaro, umbeya na upwani; tatu ni mgawanyiko wa kidini hasa mvutano kati ya waislamu na wakristo. Katika uchaguzi mkuu ujao, tunataka tuone wale wanaotaka kutuongoza wawe na kauli na majibu sahihi jinsi ya kukabiliana na migawanyiko hii. Watuambie watafanya nini na watafanyaje kutuwekea mazingira mazuri ya kulijenga taifa moja lenye umoja na hata inapolazimika kutofautiana, tufanye hivyo bila mivutano na hatari ya kuvunja umoja wetu

2- Katiba Mpya:
Hadi sasa kila mmoja wetu anafahamu kinachoendelea kuhusu mjadala wa katiba mpya. Tunajua ni kwa kiasi gani jambo hili limekua zito na gumu kwa miaka karibu mitano iliyopita. Tunajua limetumia gharama kiasi gani na tunajua ni jinsi gani limeongeza mgawanyiko mkubwa miongoni mwa watu na makundi mbalimbali ya kijamii. Tunajua ni kwa jinsi gani limeingilia mipango mingine na tunajua tuko wapi sasa hivi na nini kinaendelea.
Tunataka wanaogombea, bila kujali vyama vyao, watueleze kwa undani na uhakika wana mawazo na mipango gani ya kuhakikisha mchakato wa upatikanaji katiba mpya utafikia tamati tukiwa na umoja wa kitaifa, ushirikiano, mshikamano na kutupa majibu ya changamoto tunazotamani zitatuliwe na katiba.
3 - Umaskini: Kama taifa bado tumelemewa na umaskini kwa sehemu kubwa sana. Hata kama kuna watu wachache wenye unafuu, hatuwezi kusema nchi imeendelea wakati bado kuna mamilioni ya watu wasio na hakika ya chakula, mavazi, malazi, maji safi na huduma za afya. Wananchi tuna mamumivu makali yanayotokana na ugumu wa maisha.Tunataka kila anayegombea uongozi, atuambie kila mmoja kwa nafasi yake, ana mawazo na mipango gani ya kutusaidia kama taifa kuondokana na umaskini huu.

4: Maadili: Nchi yetu iko katika wakati mgumu sana kwa maana ya hatari kubwa ya kuzama na kuwa taifa lisilo na misingi ya maadili inayotuongoza. Kuna kila ushahidi na uzoefu wa maisha ya kawaida ya kila siku unaonesha jinsi nchi yetu imakosa misnigi ya kimaadili. Rushwa na kujuana vimekua ndio vigezo vya mambo mengi kwenye jamii yetu. Mara nyingi kama hujatoa rushwa au humjui mtu unaweza kujikuta katika wakati mgumu sana wa kupata huduma hata zile za lazima kama afya. Haki zinapatikana kwa kununuliwa. Uaminifu umekosekana kwa kiasi kikubwa. Wizi na ufisadi unaonekana kuanzia mtaani kwa wingi wa vibaka, waporaji njiani, majambazi, na matumizi mabaya ya mali za umma hata katika ofisi nyeti zinazotegemea kuwa mfano. Hofu ya watoto wadogo na vijana kwa wakubwa wao haipo tena. Heshima ya wakubwa/wazazi mbele ya watoto inapotea na mbaya zaidi wengi wa wanaojiita viongozi au waliopewa nafasi ya kutuongoza, hawana maadili hata ya kujiongoza wao wenyewe.
Anayetaka kutuongoza katika nafasi yoyote ile ana majibu na mipango gani inayotekelezeka kutukwamua katika kukosekana kwa maadili? Yeye mwenyewe ana maadili?

5 - Mapato ya taifa: Watanzania wengi na hata wageni wanaotujua, hawaelewi kwa nini sisi ni maskini. Kila wanapotazama wanaona tumezungukwa na kila aina ya utajiri na mali ambazo zingetakiwa kutuweka mahali fulani mbali na juu sana kuliko tulipo sasa. Hatuelewi ni kwanini pato la taifa liwe dogo na kwa nini bado tuendelee kuishi kwa kutegemea misaada ya wahisani.
Tunataka wagombea watueleze na kutuonesha kulijua hili kama tatizo. Watueleze ni kwa jinsi gani mali ya taifa itatumika kuongeza pato la taifa. Watuambia ni kwa jinsi gani ukwepaji mkubwa wa kodi utadhibitiwa katika nchi yetu. Kodi imekua mzigo mkubwa kwa wafanyakazi wanaojititimua kujitafutia kipato cha ujira mdogo kwa kazi kubwa na ngumu. Wakati huohuo, kuna kila dalili kwamba wengi wa matajiri na wafanya biashara hawalipi kodi kabisa au hawalipi ipasavyo. Ukusanyaji wa kodi nchini ni chini ya asilimia 20% ..ikimaanisha kama nchi ilitakiwa ikusanye shililingi mia moja basi zaidi ya 80 zinapotea na tunakusanya chini ya shilingi 20 tu. Watuoneshe wapi kuna miaya ya kodi na watakabiliana nao kwa mtindo gani na tuwape kigezo gani cha kufikia na kuwawajibisha. Tunataka watumbie pia uaminifu wao wenyewe wa ulipaji kodi kulingana na mapato na mali zao ukoje na iwapo twaweza kuthibitisha.

6 - Uwekezaji na maslahi ya Taifa: Mfumo wa uendeshaji wa nchi yetu kwa sasa sehemu kubwa unategemea uwekezaji wa ndani na wa nje. Kwa muda mrefu tumekua tukilia kwamba wawekezaji hawa hawatutendei haki. Kwanza wanapendelewa na kupewa heshima kuliko wenyeji au wasio wawekezaji na pili wanatunyonya kwa njia nyingi sana. Sheria haziwabani juu ya mishahara kwa wenyeji na wana uhuru wa kutulipa wapendavyo; wamekua wakipendelea wageni kwenye baadhi ya ajira kuliko wazawa na wakati mwingine huenda wamekua sehemu ya magenge ya wahujumu uchumi kwa kuwa wadanganyifu kwenye mapato yao na kwenye kulipa kodi.
Tunataka wanaotaka kutuongoza watuambie wanalifahamu hili kwa kaisi gani na watueleze wamejipanga kiasi gani kwa namna gani kukabiliana nalo. Watuambie ni kwa jinsi gani tutaanza kujisikia vizuri kuwa watanzania ndani ya nchi yetu na kuona fahari kwamba serikali na taifa linasimamia maslahi yetu kama ilivyo kwa nchi kama Uingereza ambayo inafanya kila linalowezekana kulinda ajira na maslahi ya raia wao kabla ya wageni

7-Utamaduni wetu: Nchi yetu haina tasfiri sahihi ya nini ni utamaduni wetu. Nilisoma makala moja katika mitandao ya inayoelezea nchi yetu kama nchi maskini kwenye tamaduni zake na moja ya sababu ni kutokuwa na hifadhi na maandishi na vitabu vihusivyo tamaduni zetu. Sina hakika ni watoto wangapi wa kitanzania wenye ujasiri wa kusimama na kueleza kwa uhakika tamaduni zetu kama taifa. Na hata kama wapo sina hakika kama kile mtoto wa Rukwa anachokijua kama utamaduni wa mtanzania ndicho atakisema mtoto wa Kagera au Bagamoyo. Nchi imepoteza mwelekeo wa kimaadili na kitamaduni na tunaiga kila tunachokutana nacho mtaani. Hatuwezi kujieleza sisi ni akina nani, tunaamini katika nini na ni nini misingi yetu kama nchi. Dira yetu ni nini na imejengwa katika nini kinachorithishwa kutoka kizazi hadi kizazi.
Tunataka wanaotuomba kutuongoza wajipange kutuambia wanawaza nini juu ya hili. Wanalijua kiasi gani na ni mzigo kwenye mioyo yao kwa kiasi gani. Kisha watuambie tunaanzia wapi kuziba ufa ambao umeshakaribia kuangusha ukuta.

9-Huduma za Jamii: Kama kuna kitu ambacho hatuna hakika nacho katika nchi yetu ni huduma za jamii. Ni watanzania wachache sana, hata miongoni mwa wale wenye fedha au mali, ambao wana hakika kwamba wiki nzima ijayo watapata umeme, watapata maji safi ya bomba, wana hakika ya kuogo kila wanapotaka, wana hakika ya huduma bora za afya wanapoumwa, wakipata tatizo la kiusalama na kisheria watapata huduma stahiki ya ulinzi, usalama na haki zao na mengine kama hayo. Tuna huduma mbovu karibu kila eneo na hakuna hata eneo moja ambalo kuna mtu mwenye ujasiri wa kusema kwa hili tumefanikiwa. Jambo hili limekua kubwa na gonjwa baya kwani hata makampuni binafsi yanayofanya biashara yameathirika na mfumo huu na wao hawajali tena wateja wao. Huduma za jamii kwenye nchi yetu zaonekana kama jambo la anasa na ikitokea umekwenda mahali ukakutana na msamaria mwema akakuhudumia unaweza kujihisi kama sio kweli vile, kama muujiza vile, ama kakupendelea, au unadaiwa au unahongwa.
Tunataka wanaotaka kutuongoza kwenye kampeni zao watuoneshe ni kwa jinsi gani matatizo haya yanawahusu wao na ni kwa jinsi gani wanautaka uongozi wakiwa na lengo la kubadilisha na kuboresha hali ilyoko. Hili linatuhusu sana na hatutaki siasa, tunataka kubadilika.

9 - Elimu: Ukiwasikiliza watu wengi utasikia malalamiko ya kushuka kwa ubora na kiwango cha elimu yetu. Utasikia tatizo la ukosefu wa elimu na mfumo wa elimu kuwa legevu. Utasikia habari za ubovu wa mazingira ya kupata elimu kuanzia shule za umma za msingi, sekondari na hata vyuo. Utasikia kilio cha kukamuliwa mamilioni ya ada kwa shule za binafsi. Utasikia kilio cha mishahara midogo na isiyolingana na hali ya maisha wala elimu waliyonayo waalimu wa shule za msingi, sekondari na wahadhiri wa vyuo vikuu. Kwa sasa kuna mjadala mzito juu ya nini kipimo cha ubora wa elimu yetu na tatizo la mkanganyiko wa lugha za Kingereza na Kiswahili ambazo zote hatuzijui wala kuzitumia kiufasaha. Utasikia kilio cha elimu kutolewa kwa upendeleo na hongo hasa kwenye vyuo vikuu. Utasikia kilio cha obovu wa wasomi wenye shahada wasioweza hata kujenga hoja wala kueleza waochokijua pamoja na kuwa na shahada zinazoitwa za daraja la kwanza.
Wanasiasa wanaotaka kutushawishi tuwachague kwenye kampeni zao wanalazimika kutonesha wanalijua hili kwa kiasi gani. Wana mipango gani na wamejipangaje kutusaidia kulitatua. Hatutaki ahadi na porojo zisizo na uhalisia. Tumechoka kuonekana wa nyuma na tusio na ujasiri kila tunapokwenda kutokana na ubovu wa elimu yetu.
Tunataka kuondoka hapa tulipo na wanawajibika kutupa majibu sahihi. Kwa wale ambao walikimbia shule lakini leo wanataka kutuongoza tusisite pia kuwauliza watatutatuliaje matatizo makubwa ya elimu katika enzi za sayansi na teknolojia huku wao wenyewe wahawajaipitia? Wanaelewa nini?

10 - Usalama. Maendeleo yoyote ya kijamii ambayo usalama wake ni wa mashaka hayana maana. Usalama ni jambo la msingi sana na linalomjengea mtu uwezo na ujasiri wa kuishi kwa faida kwake binafsi na kwa jamii. Hakuna kitu kinachokatisha tamaa kama kujua kwamba wewe na mali zako hamuko salama na kwamba kila wakati una mashaka. Usalama katika nchi yetu unadorora sana. Siku hizi ni kawaida sana kusikia makundi ya vibaka wamevamia makazi na kupora mali na kudhuru watu. Ni kawaida kusikia watu wameporwa barabarani tena mbele ya watu na katika maeneo ya wazi kabisa. Ni mazoea sasa kusikia mabenki yameporwa mchana tena kweupe na kusikia watu wametekwa na kuteswa na kuumizwa. Tuna changamoto ya ugaidia na mambo kama hayo. Usalama unapunguza muda wa kufanya kazi kutokana na hofu na unalazimisha kutumia rasilimali nyingi katika kujilinda. Zaidi sana unajenga hofu ya maisha, unaondoa furaha na kuleta msongo wa mawazo.
Wanaotaka kutuongoza wanajua nini kuhusu usalama wetu? Wamejiandaaje kubadilisha hili? Nini kimeshindikana na watawezaje kukibadilisha?

11 - Ajira. Nilisoma kauli ya Profesa mmoja wa chuo kikuu cha Dar es Salaam aliyesema taifa letu limejengwa katika misingi ya ukwepaji matatizo. Taifa la watu ambao mara nyingi hawapendi kutatua tatizo bali wanajipanga kutafuta namna ya kulikimbia. Na wanafanya hivyo kwa kutengeneza matatizo mengine.
Ukisikiliza kauli za viongozi wa nchi zote tajiri duniani hoja kubwa ni kutafutia raia wao ajira. Kuajiriwa ni jambo la msingi sana la kumpa raia uhakika wa maisha na kuchangia pato la taifa kwa kodi na uwezo wake wa kifedha. Katika nchi zao wametengeneza vituo maalum vya kusajili watu wote ambao hawana kazi na kurekodi ajira zinazotengenezwa kila siku. Wanapotoa takwimu za ajira kwamba kuna ukosefu kiasi gani au kuna ajira kiasi gani hawatoe takwimu hizo kwa kukisia au kwa kubuni au kisiasa. Wanaongea data za uhakika ambazo unaweza kuzifuatilia bila jasho. Katika nchi yetu unapoisikia takwimu za idadi ya ajira zilizopatika unajiuliza mara mia zimepatikanaje na zimepatika wapi? Ni zipi na zimebadilisha nini na kwa kiasi gani?

Tofauti na wenzetu hawa, wanasiasa wetu wanatuambia sio kazi yao kutusaidia kupata ajira badala yake twatakiwa tujiajiri. Sijajua hii kauli ilitoka wapi na alianzisha nani. Kujiajiri ni wazo jema na zuri lakini huwezi kuitumia kama hoja tangulizi mbele ya taifa la watu lenye mamilioni ya watu wasio na ajira. Ni lazima viongozi wawajibike hadi mwisho wa uwezo na mifumo ya kisera, kisheria na kiserekali kujenga kwanza miuondombinu na mazingira ya watu kujiajiri; ni lazima kuwa na mikakati ya makusudi ya serikali kuongeza ajira kunakoendana na kuongeza pato la nchi; lazima kuwe na ubunifu na uwekezaji mpya na sio kuachia soko pekee au sekta binafsi itengeneze ajira.

Ukishajenga haya mazingira wala uhitaji kuwakumbusha watu kujiajiri maana soko litawaweka mahali sahihi. Wenye uwezo wa kujiajiri na kutengeneza ajira kwa wengine watafanya hivyo na wale ambao hawana uwezo wa kujiajiri watajikuta wameajiriwa. Pia lazima viongozi watambue kwamba sio kila mwanadamu katengenezwa na vimeng'enyo vya kujiari au kuwa mfanya biashara. Hivi vitu vinaendana na mtu alivyo, elimu, upeo wa mambo na vipawa vilivyo ndani yake. Mikakati ya kulazimisha kila mtu awe mchuuzi kama njia ya kutengenza ajira haina mantiki na imewapotosha na hata kuwapoteza wengi. Ninajua watu kadhaa ambao kwa kujiingiza kwenye biashara kwa mtindo huu wamejikuta wamefilisika na kupoteza mali nyingi; wamejikuta wana madeni kwenye mabenki na hawawezi kulipa na wapo walioamua kujiua maana hawaoni kama wataweza kulipa.
Wanaotaka uongozi wanajua haya? Yana uzito kiasi gani kwao? Kwenye kampeni tunataka majibu yanayoeleweka. Wasitutolee kauli za matumaini bali watupe mipango halisia na inayotekelezeka. Hatutaki majibu ya mazoea na kauli za kutiana moyo. Hatutaki viongozi waliokariri vitabu vya manifesto za vyama vyao bali tunataka viongozi wenye uwezo wa kwenda kuzifanya manifesto hizo zitekelezeke hata kama waliotunga hawakujua wanaandika nini. Hata mwenyekiti wa kijiji ana uwezo na nafasi ya kutatua tatizo la kijiji chake kwa sehemu bila kujali chama chake kinasema nini.

12- Uwajibikaji. Watanzania tumechoka kuongozwa na wanasiasa ambao wakati wa kampeni wanatupigia magoti, wanalia machozi, wanatubusu na kutuambia wanatupenda kwa kuwa wanatafuta kura zetu. Lakini tunapowapa madaraka wanabadilika kuwa wafalme na miungu. Wanabadilika kuwa wajuaji, wasomi, wataalamu, mabingwa wa kila fani na waheshimiwa. Wanabadilika kuwa watu wasioambilika, wenye kiburi na wasiosikiliza kilio, ushauri, maonyo na mambo ya wananchi wao. Hili jambo limekua sababu ya maumivu na uchungu mkubwa sana kwa wananchi na linatupa sura na maana tofauti sana ya uongozi.

Wanaotaka kuja kutuomba kura wawe wamejiandaa. Kama wanatafuta kura zetu ili wawe watu wa namna hii juu yetu hatutawakubali. Tunataka watuambie wanakwendaje kuwa watu wa tofauti na mfumo huu. Wanakwendaje kuwa watumishi kwetu na wanaotusikiliza katika uongozi wao. Wakubaliane nasi kwamba tuwape masharti na vigezo vya utumishi na viongozi tunaowataka na iwapo watashindwa kuvifikia waturuhusu kuwawajibisha kwa kuwakataa na hata kuwaadhibu kisheria. Hatutaki viongozi wanaojiona wao ni wajuaji kuliko kila mtu kwa sababu tu tumewapa nafasi ya kutuongoza.
Vipo vilio na changamoto nyingi zinazotukabili lakini hizi nimezipa uzito maana madhara yake ni makubwa kwetu na yanasambaa kama moto wa kiangazi.
(Chanzo cha picha zote ni wavuti mbalimbali kwenye mtandao wa internet)

Mwalimu MM
Niandikie kupitia: mmmwalimu(at)gmail.comNo comments:

Post a Comment