Pages

Monday, November 16, 2015

“ Magufuli might not be the president of your choice, but he is the president, anyway!”Mwaka 2005, siku chache kuelekea ukingoni mwa uongozi wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa, alikua mgeni rasmi kwenye hafla ya kumuaga iliyoandaliwa na taasisi ya sekta binafsi (Tanzania Private Sector Foundation). Nakumbuka ilikua jioni, ameandamana na mke wake na tukio lile lilioneshwa na kituo cha ITV. Pamoja na hotuba fupi za kumpongeza na kumuaga, na zawadi alizopewa na wanachama wa taasisi hii, Mzee Mkapa alipewa nafasi ya kuongea. Nakumbuka alitoa hotuba fupi kwa lugha ya kikoloni ambayo haijaandikwa. Pamoja na kwamba sikumbuki hotuba nzima na sijafanikiwa kuipata kwenye mitandao, ila katika yale aliyongea nimekua nikikumbuka sentensi moja ambayo aliitoa huku akicheka. Ilikua na maneno yanayofanana na haya, “I might have not been the best president, but I was your president, anyway!”. Nikitafsiri kauli ile kwa lugha ya kimatumbi, alimaanisha “Inawezekana sijawa Rais mzuri sana au kama ambavyo watu walitegemea niwe, lakini pamoja na hilo bado haiondoi ukweli kwamba mimi ndio nilikua Rais wenu!”.

Mzee Mkapa alitoa kauli hii sio kwa sababu alishawishika kwamba alikua rais mbaya. Hapana. Nakumbuka alipokua anaelekea ukingoni wa urais wake, pamoja na shutuma na mambo kadhaa yaliyoibuliwa kuhusu udhaifu kwenye uongozi wake, bado alisifiwa kwa kazi nzuri aliyoifanya kwa miaka kumi hasa ya kukuza uchumi, kupunguza mfuko wa bei, kuongeza akiba ya taifa, kulipa madeni ya nje, na kuimarisha sekta binafsi. Nakumbuka watu walikua na maswali sana iwapo rais ambaye angefuata baada yake angeweza kuvaa viatu vyake na wako hata waliotoa mapendekezo kwamba kama inawezekana basi aongezewe muda. Mzee Mkapa alikua anajua sifa hizi, hivyo kauli hii naweza kuitazama kama aina fulani ya utani na majigambo ya kufurahia kazi yake. Wale waliokua wanamsikiliza walifurahi na kuangua kicheko.

Watanzania tumeamaliza uchaguzi na kwa namna yoyote ile tunayoweza kuielezea, tuna mtu ambaye kwa taratibu zetu za kikatiba, kakabidhiwa madaraka makubwa kabisa, yaani kuwa Rais wa Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania. Mtanzania huyu anaitwa John Pombe Joseph Magufuli, kwa kifupi kama JPM. Kwa kuwa uchaguzi uliopelekea yeye kuwa Rais ulikua wa vyama vingi, watanzania waligawanyika katika mchakato mzima wa uchaguzi kila mmoja akimshabikia yule aliyedhani ndio anafaa kuwa kiongozi wake. Kwa minajili hiyo, wako watu wengi, tena kwa mamilioni, ambao hawakumchagua JPM wala hawakutaka awe rais wao kwa sababu moja au nyingine.

Hata hivyo, sote kama taifa tunajua sheria za mchezo wa uchaguzi (rules of the game). Moja ya sheria hizo ambayo ni ngumu sana kuimeza, ni kwamba, mmoja akishatangazwa mshindi na kuapishwa kuwa Rais, basi sote kama taifa, hatuna budi kukubali kwamba huyo ndio kiongozi wetu. Kama moja ya mamlaka tunayomkabidhi kwa niaba yetu, mtu huyo ndiye anakua Kamanda na Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi yetu yote ya ulinzi na usalama. Wanajeshi wetu wote waliojitoa maisha yao sadaka kwa ajili ya ulinzi na usalama wetu, wanakula kiapo cha utii mbele yake. Kama vile haitoshi, mtu huyo akishaapishwa ndio anakua mkuu wa serikali na mwajiri wa watanzania wote katika utumishi wa umma. Mtu huyo ndio anabeba taswira ya nchi yetu na ndio mwakilishi wetu mbele ya uso wa kimataifa. Mtu huyo ndio anaamua aina ya utawala wa nchi uwaje na ndio mwenye mamlaka ya kuteua watu mbalimbali na kuwakabidhi majukumu ya kusaidiana naye kujenga nchi, kutoa huduma za kijamii, na kuleta maendeleo. Kama vile haitoshi, mtu huyo tunampa kibali cha kuishi na kufanya kazi kutokea jengo jeupe lililoko wilaya ya Ilala, mtaa wa Magogoni.

Kwa misingi hii ya kikatiba na kisheria, kila mtanzania, awe alimchagua JPM au vinginevyo; awe alipenda awe rais wake au vinginevyo; awe anaukubali uwezo wake wa kiungozi au vinginevyo; sote kwa pamoja, tunalazimika kumtambua, kumkubali, kumtii, kumsaidia, na kumsikiliza kama Rais wa Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania. Kwa kauli ile ya Mzee Mkapa, naweza kusema, “Bila kujali kwamba JPM ni rais mzuri au la, bila kujali tunampenda sana au vinginevyo, bado haindoi ukweli kwamba, kwa sasa, yeye ndiye Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania”. Kwa lugha ya kikoloni twaweza kusema, “Whether you chose him or not, whether you like him or not, it does not change the fact that, he is the current president of the United Republic of Tanzania, anyway!!”.

Kwa kuwa kila Mtanzania anategemewa kushiriki kuipenda na kuijenga nchi yetu; kuhakikisha kwamba taifa letu lina umoja na mshikamano; kuhakikisha kwamba tuna utulivu na tunapata maendeleo katika nyanja zote; na kuhakikisha kwamba tunalinda na kuitetea nchi yetu mbele ya maadui na wanaoinyemelea; basi kwa umoja wetu, tunalazimika kushirikiana na JMP kufanya kazi na kila mmoja kutimiza wajibu wake katika eneo lake kwa manufaa ya nchi yetu. Wale ambao hawakumchagua, ni lazima wukubali kwamba hawawezi kubadili ukweli huu kwa kuendelea kuwa na uchungu, hasira, maumivu, chuki, na mengine kama hayo kwa vile tu matakwa yao hayakutimia. Ni lazima tutoke hapo na kusonga mbele kwani tukibaki katika “mood” ya uchaguzi na “hasira ya matokeo ya uchaguzi”, hatutajitendea haki sisi wenyewe na hatutalisaidia taifa letu ambalo sote kwa pamoja tunalipenda.

Katika kitabu cha Yeremia kwenye Biblia takatifu, kuna hadithi ya wana wa Israel ambao walichukuliwa mateka kutoka nchi yao na kupelekwa utumwani Babeli. Kwa mtazamo wao, walidhani kwamba utumwa ule ambao ulitokana na maasi yao mbele ya Mungu wao, ni wa kitambo tu na Mungu atawakomboa warudi makwao mapema. Hivyo walipokua kule Babeli, waliendelea kuishi kama wapitaji maana sio kwao na hawakujiona kama sehemu ya nchi ile. Huenda wana wa Israel waliendelea kulia na kuomba usiku na mchana huku wakijipaka majivu usoni na kuvaa magunia kama ilivyokua kawaida yao wakati wa majonzi. Huenda waliendelea kulalamika na kunung’unika na kumkosoa mfalme wa Babeli na serikali yake huku wakitoa kila aina ya maneno ya laana. Hawakushiriki kuitakia mema nchi ile wala kuiendeleza kwa sababu hawakuupenda utawala uliowafanya kuwa watumwa mbali na nchi yao ya ahadi.

Ila Mungu kwa kuwa ni warehema, hata katika hali ya uasi wao, hakuwatupa na kuwasahau bali aliwawazia mema na hakuacha kutuma manabii kuongea nao. Katika hali ya kushangaa pale walipodhani Mungu anakuja kuwaokoa na kuwarudisha katika nchi yao, Mungu anamtuma nabii kuwapa ujumbe ambao bila shaka ilikua vigumu sana wao kuuelewa na kuukubali. Ujumbe huo uko katika Kitabu cha Yeremia sura ya 29. Ninakuu maneno ya ujumbe ule kuanzia mstari wa nne hadi wa saba na ule wa kumi: nayo yanasema hivi, , BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, awaambia hivi watu wote waliochukuliwa mateka, niliowafanya wachukuliwe toka Yerusalemu mpaka Babeli; Jengeni nyumba, mkakae ndani yake, kapandeni bustani, mkale matunda yake; oeni wake, mkazae wana na binti; kawaozeni wake wana wenu, mkawaoze waume binti zenu, wazae wana na binti; mkaongezeke huko wala msipungue. Kautakieni amani mji ule, ambao nimewafanya mchukuliwe mateka, mkauombee kwa BWANA; kwa maana katika amani yake mji huo ninyi mtapata Amani…. Maana BWANA asema hivi, Babeli utakapotimiziwa miaka sabini, nitawajilia ninyi, na kulitimiza neno langu jema kwenu, kwa kuwarudisha mahali hapa”.

Katika hali ya kawaida, ujumbe huu ni mgumu na mzito sana kueleweka kwa mtu ambaye anajiona kaonewa, kashindwa, ana uchungu, ana hasira, ana maumivu, na hana thamani katika mazingira aliyoko (hata kama sio kweli). Ni ngumu kukubali ujumbe huu kutoka kwa Mungu ambaye alitegemewa atasikia kilio chao na laana walizokua wanazozitoa kwa nchi ile ya ugeni wakitamani iadhibiwe. Waisrael walitamani kuona kitu kimoja tu: adhabu kwa mfalme wa Babeli na nchi yake na wao kurudi kwao. Labda waliomba watu wa Babeli watandikwe na kipindupindu kama ilivyo aina ya laana za kabila la Waibo kule Nigeria; au wote wavanmiwe na nyuki wenye sumu kali; au nchi ile itandikwe na radi ya moto mkali. Lakini kinyume na maombi hayo, Mungu anawaambia, “Acheni kalalamika na kuhuzunika. Najua muko utumwani lakini changamkeni, endeleeni na maisha, fanyeni kazi na ombeni kwa ajili ya amani na mafanikio ya Babeli. Babeli ikifanikiwa, nanyi mutafanikiwa, ikiangamia, nanyi mutaangamia, ikiwa na amani nanyi mutaishi kwa amani hadi hapo nitakapokuja kuwachukua na kuwarudisha katika nchi yenu”. Kwa kauli ya Mkapa, Mungu wao aliwaambia, “Haijalishi Babeli ni nchi yenu au la, haijalishi munapapenda au la, haijalishi muko huru au utumwani; hapa ndipo mulipo kwa sasa na maisha yenu yanategemea hali ya nchi hii”

Tanzania sio nchi ya utumwa kwetu kama ilivyokua kwa wana wa Isarel kule Babeli. Hii ni nchi yetu sote na twajisikia fahari nayo. Hivyo tuna sababu nyingi zaidi ya kuendelea kuipenda na kuitakia mema kuliko ilivyokua kwa wana wa Israel kule Babeli. Hata kama uchaguzi ulikwenda kinyume na maombi na matakwa yetu, bado maisha yetu yana thamani kubwa kuliko matakwa ya uchaguzi ambao hatuwezi kubadili kilichotokea. 
Kama ambavyo wana wa Israel waliambiwa waishi kama vile ndio wamefika na hakuna kuondoka hadi miaka sabini itakapotimia, na sisi kama watanzania, twatakiwa tusahau machungu ya uchaguzi, tumkubali rais wetu JPM na uongozi wake, tusaidieane nae kuijenga nchi na kuitakia mema: hadi uchaguzi mwingine utakapokuja tufanye maamuzi mengine kulingana na hali ya wakati huo. 


“MAGUFULI MIGHT NOT BE THE PRESIDENT OF YOUR CHOICE, AND YOU DON’T APPRECIATE HIS PRESIDENCY, BUT HE IS THE PRESIDENT, ANYWAY!!”.

Mungu ibariki Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania
1 comment:

  1. Umesema vyema mwalimu, wote kama watanzania tunaohitaji mabadiliko yatubidi kumkubali raisi tuliempata na kuendelea kusonga mbele tukizidi kuiombea nchi na raisi aliyepo kufanya maamuzi sahihi kwa maendeleo ya nchi na si wakati wakuendelea kunung'unika tena.
    Mimi ni mmoja kati ya watu naoamini yakwamba mabadiliko katika nchi yetu ya Tanzania na hata nchi nyingine zinazoendelea hususani Afrika yanawezekana.!!!!!

    ReplyDelete