Pages

Wednesday, December 30, 2015

MADHARA YA SIMU ZA MIKONONI KATIKA MAHUSIANO YA KIJAMII? SEHEMU YA KWANZA

Utangulizi na Chimbuko la Makala
Miezi kadhaa iliyopita, niliamka asubuhi na mapema kuwahi mkutano ambao nilikwenda  kuhudhuria katika jiji la London, Uingereza. Kwa kuwa nililala nje kidogo ya jiji hili lenye watu kadiri ya milioni kumi, na kwa kua ni mbali kidogo kutoka nilipokua nahudhuria mkutano, nililazimika kupanda treni kwa muda usiopungua kama dakika arobaini hadi nifike kituo cha Euston kilicho chini ya ardhi (underground) na ambapo sio mbali sana na nilipokua naelekea. Kama kawaida ya London wakati wa asubuhi, treni hujaa sana watu wakielekea makazini, kwenye utalii, na shughuli zingine. Nililazimika kusimama kwa kuwa hapakua na pa kuketi na abiria wengine wengi tu walisimama. Nilirusha macho mbele na nyuma, kushoto na kulia: na nilichokiona ni wingi wa watu waliofunikwa na ukimya wa ajabu. Sikuona mtu akiongea na mwingine wala wanaoingia wakisalimiana na wanaowakuta ndani, kitu ambacho ni tofauti sana na nilivyozoea kule kwetu uswahilini. 

Nakumbuka miaka sio mingi, kwetu uswahilini ilikua kawaida kusalimiana na kila mtu hata kama hamujuani na kama ni kwenye chombo cha usafiri munaweza kupiga stori au kujadili matukio yaliyokamata vichwa vya habari kwa uhuru na kujiachia kama vile mumelala nyumba moja au mumefahamiana kwa miaka miwili iliyopita. Kumbe, ndio kwanza munaonana kwa mara ya kwanza na hamujuani hata majina; na hadi mutakapoachana huenda hakuna atakayemuuliza mwenzake anaitwa nani au yeye ni nani au anafanya nini. Mara chache ungeweza kua na bahati ukute unayeongea naye katoka ng’ambo ya Ziwa Victoria kwani ndani ya dakika chache utajua anaitwa nani, ana shahada ngapi na za nini, na iwapo pasipoti yake imejaa au la kutokana na wingi wa safari za Ulaya na Marekani.


Pamoja na ukimya niliokutana nao, nilishangazwa na jambo moja: karibu kila niliyemtazama, alikua kainamisha kichwa akitazama simu yake na mkononi. Kila mmoja “yuko busy” kupangusa/kugusa au kubofya kioo cha simu yake. Nilipoendelea kuwaza kinachoendelea, napata ufahamu kwamba watu hawa hawako kimya, bali wako kwenye mfumo mwingine wa mazungumzo. Tofauti ya mazungumzo waliyokua wanafanya na yale ambayo nimeyazoea, ni kwamba wanaongea na ulimwengu mwingine nje na mbali ya treni tuliyokua tumepanda. Walikua wanaongea na kundi kubwa la watu na ulimwengu mpana zaidi kupitia simu visuruburu vidogo mikononi mwao, yaani simu za mkononi. Wengine walikua wanasoma; wengine “wanaperuzi” mitandao ya kijamii kama facebook, twitter, na blogs; wengine wanatuma na kusoma ujumbe mfupi; wengine wanatazama picha; na mengi mengine. Ili mradi tu kila mmoja ametekwa na taarifa/habari na mawasiliano anayofanya kupitia simu iliyo mkononi mwake.

Nilichokua nakiona asubuhi ile kilinirudisha nyuma na kunikumbusha kwamba hali ile sio ngeni na haitokei pale London tu. Nilikumbuka kwamba ni hali ambayo hata kule kwetu Msoga na Mwanaremango imekua ni kitu cha kawaida kabisa. Watu wengi hasa kundi la watu wa kipato cha kati (middle class) wenye uwezo wa kununua simu nzuri za kisasa  ziitwazao “smartphones” na kuzijaza mafuta, wamebadili sana mfumo wa mawasiliano na mahusiano. Mara nyingi hawana habari na mtu aliye pembeni mwao na kumpa umaanani kwani kupitia simu zao wanauwezo wa kuwasiliana na kuzungumza na wengi na kuona mengi kwa wakati mmoja. Ni jambo la kawaika kwenye vikao, mikutano, mafunzo na maeneo ya kungoja huduma, kuona watu wameinamisha vichwa na mikono yao imekazaka kuzungumza na visurubusu walivyonavyo mikononi. Kundi hili limewafanya hata wale wenye simu za vitufe (a.k.a kitochi) kama yangu, kujikuta nao wanalazimika kuvitazama tu na kuvibonyeza hata kama hawajui wanafanya nini. 

Hali hii ni mbaya kuliko niliyokua naiona pale London kwani angalau mule unaweza kuona walioshika vitabu vya makaratasi au wanatumia visurubusu vya kieletroniki vya kusomea vitabu (book readers): ikimaanisha waoangeza maarifa. Mara nyingine tuonapanda daladala mara kwa mara tumekua na faida zaidi kwani mazingira mule hayaruhusu kutumia, sio tu kuwasiliana na kuperuzi, bali ni hatari hata kujulikana kwamba umebeba kisurubusu hicho cha kisasa kwani wenye mji wanaweza wakaondoka nacho na sehemu ya mkono wako. Daladalani wengi twalazimika kudumisha mil ahata kama ni kwa shingo upande. Pia nilikumbuka jinsi ambayo nimepoteza marafiki na jamaa wengi ambao tunaishi karibu kabisa lakini imekua ngumu sana kuonana au kupata mazungumzo ya ana kwa ana kwa sababu tu simu za mikononi zimewezesha tundelee kuwasiliana  na kutoona umuhim wa kuonana.

Nilichokua nakiona na kumbukumbu ya kule kwetu juu ya jambo hili, ikanikumbusha  makala iliyo kwenye makavazi yangu ya kieletroniki ambayo nimekua nikiiandika kwa zaidi ya mwaka mmoja lakini kila wakati nimekua nikisita kuichapisha ili watu waisome. Mwaka mmoja na nusu hivi uliopita, nilimfuata mhadhiri mmoja wa fani ya sosholojia kumuomba nishirikiane naye kufanya utafiti kuhusu athari za simu za mikononi katika kudumisha mahusiano ya kijamii. Kwa tafsiri ya lugha ya kikoloni isiyo ya moja kwa moja niliwaza kutafiti juu ya “The use of Mobile Phones and Social Disconnection”. Lengo la wazo hili la kitafiti, lilikua ni kutazama ni kwa kiwango/namna gani simu za mikononi zinachangia kuvunja mahusiano ambayo jamii yetu ya kitanzania imekua nayo kuanzia ngazi ya familia, kindugu na hata ile ya kirafiki. Tulijadili kwa kirefu mantiki na mwelekeo wa wazo hili la kitafiti lakini tulishindwa kuanza kulifanyia kazi kwa sababu zilizokua kidogo nje ya uwezo wetu. Pamoja na kushindwa kutekeleza wazo hilo, bado niliamua kuandika makala isiyo ya kitaaluma kwa kutumia uzoefu wa niliyokutana nayo na ninayoendelea kukutana nayo kuhusu jambo hili. Hivyo nimekua nikiandika taratibu na kuweka kiporo huku nikiendelea kutafuta uhalisia wa fikra zangu kwa kufanya tafakuri pana zaidi.

Nilikua natazama mamia ya watu wale ndani ya treni jinsi walivyokua wamechotwa fikra zao na simu za mikononi huku wakiwa hawana habari na aliyekaa au kusimama pembeni yao, niliona sababu nyingine ya kunishawishi niendelee kuandika makala yangu kwa matumizi ya jamii. Nilimua kutafuta machapisho na tafiti ambazo zimefanyika sehemu zingine na kuona wanasema nini kuhusu swali nililonalo kuhusu athari za simu za mikononi. Nimefurahi kukuta tafiti kadhaa zimeongelea eneo hili ingawa zimetazama zaidi athari azipatazo mtu binafsi.

Makala hii imedhamiria kuchambua ukweli wa jambo hili na kupendekeza mambo kadhaa kama sehemu ya kutafuta suluhisho la kijamii kwa mtu mmoja mmoja. Endelea kusoma sehemu zitakazofuata kupitia jukwaa hili .Pia waweza kuniandikia kupitia 

Taadhari: Chanzao cha picha zote ni mtandao wa internet.  

Mwalimu MM
mmmwalimu@gmail.com

No comments:

Post a Comment