Pages

Monday, January 4, 2016

MADHARA YA SIMU ZA MIKONONI KATIKA MAHUSIANO YA KIJAMII? SEHEMU YA PILI

Kwa nini simu za mikononi ni tishio kwa jamii yetu?
Katika makala hii na zitakazofuata, ninapotumia neno matumizi ya simu za mkononi, ninamaanisha mawasiliano ya kupiga na kupokea simu; utumaji na upokeaji wa ujumbe mfupi wa simu (SMS); matumizi ya mitandao ya kijamii kupitia simu; kucheza games kupitia simu; kutuma na kupokea barua pepe; na matumizi mengine ya intaneti kupitia simu.

Tangu kugunduliwa kwa teknolojia ya simu za mikononi, imekua na kuenea/kusambaa kwa haraka sana duniani kuliko teknolojia nyingine yoyote ile ambayo imewahi kugunduliwa katika historia ya mwanadamu. Kwa mfano: wakati ugunduzi wa runinga umetokea miaka kama 100 iliyopita, Tanzania bara tumeanza kutazama runinga kama miaka 25 tu iliyopita. Kulingana ya repoti ya mwisho wa mwaka 2014 ya Mamalaka ya Mawasiliano nchini (TCRA), Tanzania nzima kuna wastani wa runinga 1,000,000 pekee. Simu za mezani (landline au za TTCL) zimegunduliwa kwa mara ya kwanza na mskotishi Alexander Graham Bell mwaka 1876 lakini hadi mwezi wa tisa mwaka huu ni wateja (subscribers) takribani 304,000 pekee ndio wanamiliki simu hizi. Hali kadhalika, wakati ugunduzi wa internet umetokea miaka ya 1960, Tanzania tumeanza kutumia internet mwishoni mwa miaka 1990 tena kwa watu wachache sana. Hadi mwezi wa tisa mwaka 2015 ni takribani watu 1.9M pekee ndio wanamiliki (subscribers) huduma hii ikiwa ni pamoja na maofisi. Mashine za kufulia nguo (washing machines) zimeanza kutumika nchini Sweden mwanzoni mwa miaka ya 1950 lakini hadi sasa watanzania wanaotumia teknolojia hii kama kifaa cha nyumbani ni wa kutafuta na huenda kuna mikoa haina hata mashine moja. Usambazaji umeme umefanyika kwa mara ya kwanza nchini Uingereza mwaka 1881 lakini hadi leo miaka 135 baadaye, umeme ni huduma ya anasa Tanzania na umewafikia watu chini ya 40%.