Pages

Monday, January 4, 2016

MADHARA YA SIMU ZA MIKONONI KATIKA MAHUSIANO YA KIJAMII? SEHEMU YA PILI

Kwa nini simu za mikononi ni tishio kwa jamii yetu?
Katika makala hii na zitakazofuata, ninapotumia neno matumizi ya simu za mkononi, ninamaanisha mawasiliano ya kupiga na kupokea simu; utumaji na upokeaji wa ujumbe mfupi wa simu (SMS); matumizi ya mitandao ya kijamii kupitia simu; kucheza games kupitia simu; kutuma na kupokea barua pepe; na matumizi mengine ya intaneti kupitia simu.

Tangu kugunduliwa kwa teknolojia ya simu za mikononi, imekua na kuenea/kusambaa kwa haraka sana duniani kuliko teknolojia nyingine yoyote ile ambayo imewahi kugunduliwa katika historia ya mwanadamu. Kwa mfano: wakati ugunduzi wa runinga umetokea miaka kama 100 iliyopita, Tanzania bara tumeanza kutazama runinga kama miaka 25 tu iliyopita. Kulingana ya repoti ya mwisho wa mwaka 2014 ya Mamalaka ya Mawasiliano nchini (TCRA), Tanzania nzima kuna wastani wa runinga 1,000,000 pekee. Simu za mezani (landline au za TTCL) zimegunduliwa kwa mara ya kwanza na mskotishi Alexander Graham Bell mwaka 1876 lakini hadi mwezi wa tisa mwaka huu ni wateja (subscribers) takribani 304,000 pekee ndio wanamiliki simu hizi. Hali kadhalika, wakati ugunduzi wa internet umetokea miaka ya 1960, Tanzania tumeanza kutumia internet mwishoni mwa miaka 1990 tena kwa watu wachache sana. Hadi mwezi wa tisa mwaka 2015 ni takribani watu 1.9M pekee ndio wanamiliki (subscribers) huduma hii ikiwa ni pamoja na maofisi. Mashine za kufulia nguo (washing machines) zimeanza kutumika nchini Sweden mwanzoni mwa miaka ya 1950 lakini hadi sasa watanzania wanaotumia teknolojia hii kama kifaa cha nyumbani ni wa kutafuta na huenda kuna mikoa haina hata mashine moja. Usambazaji umeme umefanyika kwa mara ya kwanza nchini Uingereza mwaka 1881 lakini hadi leo miaka 135 baadaye, umeme ni huduma ya anasa Tanzania na umewafikia watu chini ya 40%.


Kinyume na hayo yote, teknolojia ya simu za mikononi imeanza kutumika rasmi mwishoni mwa miaka ya 1980 lakini haikuchukua miaka kumi ikawa imeshaingia nchini kupitia makampuni kama ya Traitel, Mobitel na mengine. Kutokana na taarifa za TCRA, hadi mwezi wa sita mwaka 2015 kuna watumiaji wa simu (yaani SIM cards zilizoko zinazotumika) milioni 35.6. Unaweza kuona ni kwa jinsi gani simu za mkononi zimekua sehemu ya maisha ya watanzania. Teknolojia hii imekuza na kuboresha mawasiliano na upatikanahi wa taarifa kwa kiasi kikubwa. Simu za mikononi kuweza kutumia internet imechagia zaid ongezeko la matumizi yake na kubadilisha kabisa dhana nzima ya mawasiliano katika jamii.  

Tafiti nyingi za kisayansi zimefanyika kote duniani kuhusu matumizi ya simu. Hata hivyo, tafiti nyingi zilizofanyika katika mazingira ya nchi kama zetu (nchi za dunia ya tatu) kuhusu matumizi ya simu za mikononi, zimejikita katika kutazama faida zake na jinsi ya kuzitumia kukabiliana na changamoto mbalimbali kama vile kurahisisha mihalama ya fedha; mawasiliano na utoaji wa huduma za afya; ufanyaji biashara; na utafutaji wa masoko na bidhaa. Hali kadhalika, nyingi ya hizi tafiti zimejikita zaidi katika teknolojia yenyewe na inavyofanya kazi huku machache yakisemwa kuhusu uhusiano wa teknolojia ya simu za mikononi na maisha ya kila siku ya watu na tamaduni zao.

Kwa nini ni muhim kutazama athari za teknolojia na maisha ya jamii?
Tafiti zinaonesha kwamba kila teknolojia mpya inapogundulika kunakua na athari zake katika maisha ya watu kulingana na inapotumika. Matumizi ya simu za mikononi katika upashanaji habari na mawasiliano yameingilia sana aina ya maisha na mahusiano ya kijamii tuliyokua nayo kama jamii ya kitanzania. Ni wazi kwamba jamii haiwezi kuwa imebaki vilevile ilivyokua baada ya kumkaribisha mgeni huyu (simu) ambaye kwa kwa wengi amekua kampani na mshikaji mkubwa hata kuliko ndugu, jamaa, marafiki na wapenzi.  Ikumbukwe kwamba, kwa jamii za kitanzania, wako watu wengi sana ambao simu ya mkononi ndio teknolojia ya hali ya juu kabisa wao kuiona na kuitumia tangu kuumbwa kwa misingi ya dunia, achilia mbali kuimiliki. Hali hii iko hivi wakati huko zilipotoka, maendeleo ya teknolojia mbalimbali yamekua sehemu ya kawaida ya maisha yao kwa miaka mingi iliyopita. Hivyo mshtuko wa mgeni simu kwao hauwezi kufanana na hapa kwetu. Wakati faida za simu kama teknolojia zaweza kufanana popote inapotumika, athari zake kwa jamii ya kitanzania zinaweza zisifanane kabisa na athari wazipatazo jamii za kimagharibi kutokana na tofauti ya misingi inayofanya familia na jamii husika.  Kwa nini na kivipi? 

Misingi ya kitamaduni na kijamii inatofautiana kati ya jamii moja na nyingine na kati ya nchi na nchi. Misingi na taratibu hizi za kijamii au kitamaduni, ndizo ambazo kwa sehemu kubwa zinaamua aina ya maisha watu wanayoishi na inaathiri (hasi au chanya) karibu kila eneo la mahusiano, uzalishaji, uwajibikaji, huduma za jamii, na mambo mengine. Jinsi tulivyo ni akisi ya jamii na mazingira yanayotuzunguka na mazingira haya yanapobadilika au kuvamiwa, kuna kila uwezekano wa kuyafuata mabadiliko hayo hata kama hatujui yanapotupeleka. Siku moja nilipanda Taxi katika mji mmoja nje ya nchi iliyokua inaendeshwa na raia mwenye asili ya kiasia. Kwa kuwa nilikua ninakwenda mbali kidogo, tulizungumza mambo kadha wa kadha. Nilimuuliza swali kwamba ni kwa nini pamoja na yeye na wengine niliowaona kua wazaliwa wa nchi ya Ulaya lakini wamekumbatia tamaduni za kiasia kama vile wako kwao. Alinijibu kwa ufupi kwamba, uraia wa nchi ni utii (loyalty) mtu alio nao kwa nchi yake, lakini utamaduni wake ndio utambulisho wake. Alimaanisha kwamba akiacha utamaduni wake basi anakua hana utambulisho tena (no identity). Unaweza kuwa raia wa nchi yoyote duniani lakini asili yako haibadiliki na inapobadilika basi unakosa utambulisho. Kwangu nikaona anachomaanisha ni pamoja na kutazama ni kwa kiasi gani, tumejiandaa kukabiliana na mabadiliko kama ya teknolojia yanayoweza kuathiri jamii na utambulisho wetu. Nitatoa mifano mitatu ya makundi ambayo nitajikita kuyachambua baadaye: 

Moja: Katika jamii za kimagharibi dhana ya ndoa ni jambo la kibinafsi sana na linamtegemea mtu binafsi kuamua nini cha kufanya kuhusu maisha yake. Vijana au watu wazima wanaweza kujiamulia kuwa na mahusiano ya kimapenzi kwa miaka nenda rudi bila kujadili au kugusia ndoa. Sheria zinawalinda kuhusu uhuru wa kuzaa au kutoa mimba. Ndoa inaweza kuwa mkataba wa muda mfupi au mrefu wenye masharti nafuu au magumu. Na mengine mengi. Kwa upande wa pili, jamii zetu pale Sinza au Ngaramtoni au Uyole kule Mbeya, zina mtazamo tofauti sana kuhusu ndoa. Ndoa ni kitu cha kuheshimiwa na watu wote na ni jambo la kifamilia na jamii yote. Heshima ya ndoa ina nafasi ya kipekee katika jamii na hivyo mchakato wa kuingia na kutoka kwenye ndoa ni mrefu na unahusisha watu wengi. Dini ni sehemu kubwa ya mahusiano ya ndoa na hata wasio na dini wanafungwa na taratibu za kifamilia, kimila na kijamii. Pamoja na kwamba watu wana uhuru wa kuishi wapendavyo, lakini taratibu za kijamii zinawasuta na hawapati amani ya kutosha kuishi au kufanya mambo nje ya taratibu hizo. Kuvunja ndoa (kuacha au kuachika) sio jambo la kishujaa bali ni aibu na jambo la kufedhehesha kwenye jamii yetu.

Mbili: Mtoto anayelelewa mazingira ya tamaduni za kiamerika au Uaya, anaona na anafundishwa tangu akiwa mdogo kabisa kwamba maisha yake ni yake mwenyewe na anatakiwa kujitegemea na kujitazama katika ubinafsi wake bila kujali ndugu, jamaa au jirani. Mahusiano na mawasiliano yake mengi yamejikita katika muingiliano na vifaa vya mawasiliano (simu, internet), katuni, mziki, filamu, na michezo au vitu vinagine vinavyomfurahisha. Mtoto akikosea huruhusiwi kumwadhibu na badala yake utanyamaza tu kama mdomo umechoka kuonya na utakapoamua kunyoosha mkono, basi atatazama ilipo simu awajulishe polisi au amwambie jirani na ndani ya dakika chache utakua mikononi mwa pilato kungoja mchakato wa hukumu. Kwa upande mwingine, mtoto anayekulia pale Mtama kwa mheshiiwa Waziri Nape Nnauye au Iramba kwa Kaka yangu Mwigulu Madelu mwana wa Nchemba, tunamfundisha dhana ya udugu, ujamaa, kuheshimu wakubwa, kusaidia ndugu, na mengine kama hayo. Mtoto huyu akikosea tuna uhuru wa kumuonya kwa adhabu (isiyolenga kumuumiza) na anaweza kupewa mwongozo au kuonywa na mtu mzima yeyote atakayemkuta katika mazingira yasiyostahili. Mzazi wake anaongozwa na dhana aliyotufikirisha Mama Salma wa Kikwete, kwamba, “mtoto wa mwenzio ni wako” na hivyo kwa sehemu moja au nyingine unawajibika na usalama, makuzi, na mahitaji yake ili kujenga jamii bora na yenye mshikamano zaidi.

Tatu: Kijana wa kike na wa kiume aliyekulia katika mataifa ya kimagharibi akishafikisha umri wa miaka kama kumi na sita, sheria inamlinda kwamba sasa anaweza kujiamulia atakayo, kuishi apendapo, kunywa au kutokunywa pombe, kuendelea kuishi na wazazi wake au kwenda mtaani kwa washikaji, kulala kwa rafiki wake wa kiume au wa kike bila kuomba kibali wala kuhojiwa; kuendelea na shule au kusema sitaki niatauza baga. Hakuna mtu wa kumuadhibu na ukimnyooshea mkono, jela inakusubiri kwa kosa la “domestic violence” au “physical abuse”. Kwa upande mwingine, kijana wa kule kwetu umatumbini na uzaramoni, amekua akijua kwamba anawajibika kwa wazazi, familia, na jamii inayomzunguka. Tumemkuza akijua dhana ya uwajibikaji na kujiheshimu mbele ya jamii na kwamba aibu yake ni aibu ya wote. Anajua anawajibika kuheshimu wazazi na hatakiwa kujenga mahusiano machafu au kujihusisha na tabia mbaya kama za ulevi, uvutaji, madawa ya kulevya, ujambazi, ngono, na ukorofi mwingine. Tumemfundisha misingi ya kumpenda Mungu na kufuata taratibu za dini zenye kulenga kumfanya kuwa mtu mwema katika jamii. Anajua kwamba siku moja analazimika kuhusika na hali za wadogo zake na familia kw aujumla na kutoa mchango wa makuzi zliyoyapata.

Niweke kumbukumbu sawa kwamba haya niyoyataja hayafanyiki kwa utimilifu wa niliyoyaeleza, ila hiyo ndio misingi inayotuongoza bila kujali tunaifuata au tunaikiuka kwa kiasi gani. Kwa kuyatazama mifano hii, ni wazi kwamba tutarajie athari za kijamii pale unapoleta mgeni king’ang’anizi aitwaye simu ambaye ameichota jamii kifikra, hisia, na vipaumbele. Hali inaweza kuwa tofauti au athari kuwa ndogo kwa wenzetu kule magharibi kutokana na mfumo wao wa maisha, lakini ni wazi kwamba sisi tunakwenda tusikokujua. 

Je, tafiti za kisayansi zinasema nini kuhusu athari za simu za mikononi katika akili zetu, hisia (emotions) zetu, mahusiano yetu, na uwezo wetu kwa kufanya na kukumbuka mambo? Nitaliongelea hili katika makala inayofuata.

Endelea kusoma sehemu zitakazofuata kupitia jukwaa hili. 

(Tahadhari: Chanzo cha picha zote ni mtandao ya internet)

Mwalimu MM
mmmwalimu(at)gmail.com

No comments:

Post a Comment