Pages

Saturday, January 14, 2017

NI NJIA GANI ITAYOKAYOKUHAKIKISHIA USALAMA NA USIRI WAKO WAKATI WA MAWASILIANO?

Utangulizi:
Usiri (confidentiality) na usalama (security) ni dhana na bidhaa mbili zenye umuhim mkubwa sana kwenye mawasiliano kwa njia za kielekroniki kama simu, ujumbe mfupi wa maandishi, na baruapepe (emails). Moja, ni uhakika kwamba nikiongea na mtu kwa simu au kwa ujumbe wa maandishi (SMS au programu zingine zinazoruhusu kuchati) au kwa baruapepe (emails) hakuna mtu mwingine asiyehusika ambaye anaweza kuyasikia au kuyaona mawasiliano yangu (confidentiality). Mbili, ni uhakika kwamba ninapofanya mawasiliano, mtu au watu wenye lengo la kufuatilia mawasiliano yangu hawataweza kufanya hivyo kwa kuwa nina ulinzi dhidi ya kuingiliwa (kusikiliza sauti au kuona ujumbe) mawasiliano yangu (Security). Haya mambo mawili ni mahitaji makubwa kwa mteja yeyote wa huduma ya mawasiliano duniani kote.

Jinsi mawasiliano ya simu yanavyoweza kuingiliwa.  Chanzo: mtandao wa Internet 

Sio lengo la makala hii fupi kukuchosha kwa kuongea kwa undani utaalamu na teknolojia za mawasiliano na jinsi zinavyofanya kazi bali nataka tu kumishirikisha elimu kidogo kwa wale wasio na uelewa wa kutosha na hivyo kumisaidia mambo kadhaa: moja, kujua njia sahihi ya kutumia kulingana na aina ya mawasiliano; mbili, kujua njia gani sio sahihi kuwasiliana wakati gani; tatu, kujua jinsi ya kujilinda na kujihakikisha usalama na usiri kwenye mawasilinao; na nne, kuwa na ujasiri au kujiamini unapowasiliana kwamba uko salama. Hali kadhalika, inaweza kumisidia baadhi ya watu kujua ni aina gani ya simu au vifaa vingine wanavyohitaji kulingana na asili ya mawasiliano yao. Hata hivyo, makala hii haina lengo la kumshawishi au kumsaidia mtu kufanya uhalifu na kuvunja sheria zihusianazo na makosa ya mawasilinao ya kimtandao.