Pages

Wednesday, March 1, 2017

Matumizi ya simu wakati wa kuendesha gari: moja ya tishio jipya la maisha duniani

Siku za karibuni tumeona hatua ya jeshi la polisi kutumia ushahidi wa picha na video za mitandaoni katika kufuatilia makosa ya madeva barabarani. Jambo hili ni la kupongezwa sana na kuunga mkono. Watu wengi hupenda kupiga picha za kujidai wakiwa wanaendesha magari huku wakiwa hawajafunga mikanda, wanatumia simu kujirekodi, nk, na haya sio mambo ya kuvumilia kwa nchi inayotaka kufuata sheria na taratibu zilizowekwa. Ningetamani kitengo cha mitandaoni cha jeshi la polisi kichukue hili kama moja ya jukumu la ufuatiliaji na wasiishie kwa wale tu ambao wamejulikana kama Diamond. Nataka nizungumzie moja ya makosa haya na nitatoa mfano wan nchi moja ambayo kwa sehemu kubwa tumerithi mfumo na sheria zao
Dai1.jpg 
Ajali za barabarani zinazotokana na matumizi ya simu za mikononi wakati wa kuendesha gari zimeongezeka sana duniani kote na zinagharimu maisha ya watu wengi sana na kuacha wengi wakiwa vilema na upotemvu mkubwa wa mali. Nchi nyingi duniani zinabuni hatua mbalimbali za kupunguza tatizo hili. Pamoja na elimu kubwa kwa raia, matangazo barabarani, na mafunzo mbalimbali, wanaweka sheria ngumu ili kupunguza uwezekano wa madereva kufanya makosa. Sina hakika iwapo nchi yetu tuna rekodi sahihi za ajali zinazohusianishwa na utumiaji wa simu hasa kutokana na ukweli kwamba hatuna mifumo mizuri ya kutunza taarifa, kuchunguza, na kuthibitisha vyanzo vya ajali kwa vielelezo. Pia kuna shuhuda nyingi ya sababu za ajali kuandikwa kinyume na chanzo halisi kwa sababu ambazo nisingependa kuzitaja hapa. Ila iwavyo vyovyote vile, kuna ajali nyingi sana zinasababishwa na matumizi ya simu kwa madereva. Jambo hili linahitaji kuchukuliwa kama janga na kupewa uzito wa kutosha tukianzia na elimu kwa jamii kukubali kubadilika na kuacha kuwa watumwa wa mawasiliano hata pale isivyo lazima. Ni lazima kila anayeendesha gari ajishawishi kutotumia simu na raia wawe wakali wanapoona dereva anafanya hivyo. Tafiti nyingi zilizofanyika nchi nyingi duniani zimeonesha kwamba matumizi ya simu wakati wa kuendesha gari yanamwondoa dereva katika umakini (concentration) ya kinachoendelea barabarani na hivyo kumweka katika hatari kubwa ya kufanya makosa au kushindwa kuchukua hatua kwa wakati pale inapojitokeza hatari.