Pages

Wednesday, March 1, 2017

Matumizi ya simu wakati wa kuendesha gari: moja ya tishio jipya la maisha duniani

Siku za karibuni tumeona hatua ya jeshi la polisi kutumia ushahidi wa picha na video za mitandaoni katika kufuatilia makosa ya madeva barabarani. Jambo hili ni la kupongezwa sana na kuunga mkono. Watu wengi hupenda kupiga picha za kujidai wakiwa wanaendesha magari huku wakiwa hawajafunga mikanda, wanatumia simu kujirekodi, nk, na haya sio mambo ya kuvumilia kwa nchi inayotaka kufuata sheria na taratibu zilizowekwa. Ningetamani kitengo cha mitandaoni cha jeshi la polisi kichukue hili kama moja ya jukumu la ufuatiliaji na wasiishie kwa wale tu ambao wamejulikana kama Diamond. Nataka nizungumzie moja ya makosa haya na nitatoa mfano wan nchi moja ambayo kwa sehemu kubwa tumerithi mfumo na sheria zao
Dai1.jpg 
Ajali za barabarani zinazotokana na matumizi ya simu za mikononi wakati wa kuendesha gari zimeongezeka sana duniani kote na zinagharimu maisha ya watu wengi sana na kuacha wengi wakiwa vilema na upotemvu mkubwa wa mali. Nchi nyingi duniani zinabuni hatua mbalimbali za kupunguza tatizo hili. Pamoja na elimu kubwa kwa raia, matangazo barabarani, na mafunzo mbalimbali, wanaweka sheria ngumu ili kupunguza uwezekano wa madereva kufanya makosa. Sina hakika iwapo nchi yetu tuna rekodi sahihi za ajali zinazohusianishwa na utumiaji wa simu hasa kutokana na ukweli kwamba hatuna mifumo mizuri ya kutunza taarifa, kuchunguza, na kuthibitisha vyanzo vya ajali kwa vielelezo. Pia kuna shuhuda nyingi ya sababu za ajali kuandikwa kinyume na chanzo halisi kwa sababu ambazo nisingependa kuzitaja hapa. Ila iwavyo vyovyote vile, kuna ajali nyingi sana zinasababishwa na matumizi ya simu kwa madereva. Jambo hili linahitaji kuchukuliwa kama janga na kupewa uzito wa kutosha tukianzia na elimu kwa jamii kukubali kubadilika na kuacha kuwa watumwa wa mawasiliano hata pale isivyo lazima. Ni lazima kila anayeendesha gari ajishawishi kutotumia simu na raia wawe wakali wanapoona dereva anafanya hivyo. Tafiti nyingi zilizofanyika nchi nyingi duniani zimeonesha kwamba matumizi ya simu wakati wa kuendesha gari yanamwondoa dereva katika umakini (concentration) ya kinachoendelea barabarani na hivyo kumweka katika hatari kubwa ya kufanya makosa au kushindwa kuchukua hatua kwa wakati pale inapojitokeza hatari.


simu.jpg 

Leo nchi ya Uingereza imeanza kutekeleza upya sheria ya usalama barabarani juu ya matumizi ya simu ukiwa unaendesha gari. Kabla ya leo, ulikua ukikamatwa unatumia simu ukiendesha gari ulikua unatozwa faini ya £100 (laki 3 za Tz) na leseni yako inaongeza alama (points) 3 za makossa (Kumbuka points za makosa ya barabarani zikifika 12 unapoteza leseni yako). Kuanzia leo ukikamatwa na kosa la kutumia simu unatozwa faini ya £200 (kama laki 6 za Tz) na leseni yako inaongeza alama (points) 6 za makosa. Kwa dereva mwenye leseni yenye miaka chini ya miwili (tangu uipate kwa mara ya kwanza) ukikamatwa na kosa hili unapoteza hiyo leseni hapohapo na kuipata tena inabidi ukaanze kuitafuta kuanzaia hatua ya kwanza ya mitihani kama nitakavyogusia mbeleni na mchakato huu unachukua muda mrefu. Sheria hii inawaruhusu hata raia watakapoona dereva anatumia simu akiendesha au anasubiri kwenye mataa kupiga picha na kuwatumia polisi na zitatumiwa kumweka hatiani. Mtu unaruhusiwa kutumia simu pale tu unapolazimika kupiga polisi (number 999 pekee) kuomba msaada katika mazingira hatarishi kama vile unapokimbizwa na majambazi.

Uingereza ni moja ya nchi zenye sheria ngumu na kali sana ya usalama barabarani. Leseni yake inaheshimika na inakubalika na nchi zote duniani pamoja na kwamba ni nchi hii na nchi zingine chache sana duniani (ikiwemo Tanzania) zinaendesha gari upande wa kushoto (keep left). Kupata Leseni ya udereva Uingereza ni zoezi gumu, la muda mrefu na la gharama kubwa sana. Madesa unayotakiwa kusoma kujiandaa na mitihani ya kupata leseni ni kama mtu anayefanya mtihani wa kuhitimu elimu ya kiwango cha cheti maana ni mengi sana na alama za barabarani ni nyingi sana. Kupata leseni utakiwa kufanya mtihani wa nadharia (theory) ambao ni automated na ukimaliza unafanya mtihani wa pili unaoitwa Hazard perception test ambao ni mgumu kuliko wa kwanza maana ndio unafelisha watu wengi katika hatua hii. Huu ni mtihani wa computer simulation na unalenga kukupima iwapo una uwezo wa kuelewa mazingira ya uwezekano wa kutokea ajali barabarani kabla haijatokea na kuchukua hatua sahihi.

Ukifaulu mitihani hii miwili (unafanya ndani ya siku moja na majibu unayapata baada tu ya kutoka chumba cha mtihani) ndio unaruhusiwa kwenda kulipia kwa ajili ya mtihani wa vitendo (practical test). Kwenye vitendo unajaribiwa kwa dakika 40 barabarani ukitakiwa kufanya manoeuvring nyingi/mbalimbali na uwezo wa kufuata sheria nyingi na matumizi sahihi ya barabara za aina tofautitofauti. Unapomaliza mtihani huu na kupaki gari yatari unapewa matokeo hapohapo kujua kama umefaulu au hapana. Aina ya leseni utakayopewa iwapo umefaulu hatua hii ya pili, inategemea aina ya gari ulilokwenda nalo kufanyiwa mtihani na wewe ndio muamuzi. Ukifeli mtihani wa nadharia utalipia na kurudia hata mara kumi hadi ufaulu ndio uweze kujisajili na kulipia mtihani wa vitendo. Nao ukishindwa utaendelea kulipia na kurudia hadi utakapofaulu. Hakuna huruma, hakuna rushwa, hakuna njia ya mkato na taratibu zote hizi ziko centrally controlled na mamlaka inayohusika na usafiri (DVLA). Kama kuna mitihani inayoweza kukumiza kichwa kwa stress yake ni hii ya kupata leseni (natharia na vitendo) na examination process yake ngumu na strict sana.

Nchini Uingereza kama kuna makosa yanaweza kukulaza macho na kukugharimu sana kwenye maisha yako kwa ujumla ni makosa ya barabarani. Ukifanya kosa barabarani, pamoja na adhabu unayopata, kosa hilo laweza kukunyima kupata baadhi ya kazi, litaongeza bima ya gari na kwenye karibu kila eneo kwa muda mrefu, na kuna vitu unaweza kuvikosa kabisa kulingana na aina ya kosa. Kuna makosa kama ya kuzidisha mwendo ambayo unatozwa faini kubwa na kuongeza points kwenye leseni. Mengine unatozwa faini za hadi £2500 (Milioni 7 za Tz) na unakwenda jela. Pia yako ambayo unatozwa faini, unakwenda jela, na hutaendesha gari tena kwa miaka kadhaa au hadi ufariki. Kuna mengine utalazimika kufanyiwa mafunzo maalumu nyingine ya polisi (kwa gharama kubwa) kabla ya kurudishiwa tena leseni yako.

Pamoja na kwamba kuna ajali nyingi barabarani (sababu ziko nyingi) sheria zao ngumu kwa sehemu kubwa zimesaidia sana ustaaribu wa hali ya juu barabarani. Nchi hii ina watu kama Milioni 70 na inakadiriwa kila mtu ana magari mawili hivyo makadirio ya jumla ya magari milioni 120. Wakati huohuo Uingereza ni nchi ndogo sana kwani mara nne yake ndio unapata ukubwa wa nchi ya Tanzania. Magari yanayopita kwenye barabara kubwa moja tu kwa siku (Motorways) kama vile M1 au M6 yanaweza kuzidi magari yote Tanzania. Sina data za karibu lakini sidhani kama nchi yetu imefikisha hata magari milioni 2. Data zilizoko WHO zinaonesha mwaka 2011 tulikua na magari yaliyosajiliwa 977,468 na kutokana na habari iliyo kwenye blog ya Millard Ayo ya mwaka 2014 Tanzania ilisajili jumla ya magari mapya 226,806 kwa miaka mitano (mwaka 2008 hadi 2013). Uingereza inasajili magari mapya 600,000 kila mwaka.

Kwa idadi ndogo ya magari tuliyonayo tunaweza kupunguza sana ajali zitokanazo na matumizi ya simu za mikononi kama kila dereva atakuwajibika. Jambo hili linahitaji zaidi ya sheria. NI alazima eleimu ya udereva iendane na msisitizo wa mafunzo ya makatazo kwa mareva ikiwa ni pamoja na hili. Jeshi ya polisi na vyombo husika vitoe elimu ya kutosha kwa kuhusisha jamii nzima ya kuoensha ni kwa jinsi gani jambo hili ni hatari kwa maisha na kila mmoja anatakiwa kuwa msimamizi na mtekelezaji wa sheria hii. Hata hivyo umakini wa ufuatiliaji wa makosa ya barabarani kama hili na mengine hauwezi kufanikiwa kwa mfumo wa usimamizi wa sheria tulionao sasa hivi unaotegemea wingi wa traffic police barabarani. NI vema jeshi letu litumie baadhi ya mapato makubwa wanayokusanya kwa sasa kupitia makosa barabarani, kuwekeza kwenye usalama ikiwa ni pamoja na kuweka surveillance camera, kamera za mwendokasi zisizotegema uwepo wa askari, na kutumia mifumo ya TEHAMA katika kukusanya, kutuma, na kuhifadhi taarifa zihusianazo na matumizi ya barabara. Hili liendane na uwepo wa sera na sheria sahihi ili isionekane kama ni ukomoaji na ukali uliopitiliza kwa raia, bali sehemu ya ustaarabu wetu kama taifa lilielimika na linalofuta taratibu zake kulinda maisha, afya, na mali za watumiaji wa barabara.

(Muhim: Chanzo cha picha zote ni mtandao wa internet)

Mwalimu MM
mmmwalimu(at)gmail.com

No comments:

Post a Comment