Pages

Thursday, May 11, 2017

Unywaji wa kahawa unaweza kukukinga na magonjwa ya moyo

UTANGULIZI: Makala hii fupi ya kisayansi tuliandika mwakaa 2015 na kuomba kuichapisha kwenye magazeti kadhaa ya Tanzania kwa kuwa tulijua sio watu wengi watakaoweza kuusoma huo utafiti na kufaidi yaliyomo. Pia tuliona utafiti huu ni chachu kwa nchi yetu hasa kutokana na ukweli kwamba kahawa ni moja ya mazao muhim ya biashara nchini.

Hata hivyo magazeti yote tuliyoomba walitukatalia maana hawakua na interest nayo na wengine hawakutujibu kabisa (Ni ngumu sana kupata nafasi ya kuandika makala kwenye magazeti yetu hasa kama hakuna mtu anayekufahamu kwenye chombo husika).

Baada ya kukwama tuliamua kuiweka kwenye blog ya www.wavuti.com. Lakini kwa umuhim na uzito wa utafiti huu wa Bwana Choi na wenzake, nimeona ni vema niweke tena hapa andiko hili ili kuwapa nafasi wanaotembelea kurasa hizi maarifa ya kuwasaidia na wawashirikishe wengine. Karibu ujisomee.


Khawa.jpgUtafiti uliofanywa nchini Korea na mtafiti Choi na wenzake na kuchapishwa mwezi Machi kwenye jarida la kisayansi liitwalo Heart, umechangia sana kuondoa utata uliokuwepo kwa muda mrefu kuhusu ubora au madhara ya kiafya yatokanayo na unywaji kahawa. Utafiti huo ambao ni mkubwa sana ulihusisha zaidi ya watu elfu ishirini na tano (25,000) umeonesha unywaji wa kahawa hadi vikombe 5 kwa siku husaidia kupunguza maradhi ya moyo.Kahawa inajulikana kwa kuongeza kasi ya mapigo ya moyo kitu ambacho kinaweza kuchangia kuongeza shinikizo la damu, lakini pia kahawa husaidia kushusha shinikizo la damu kwa kupanua mishipa ya damu mwilini na kupunguza maji mwilini kwa kupitia mkojo. Wataalamu wengi wa afya kwa muda mrefu wameshauri kinyume na unywaji wa kahawa na kuonya kwamba inaweza kupelekea kuleta magonjwa ya moyo.

Shirika la kukinga na maradhi ya moyo nchini Marekani (American Heart Society) liliwahi kutoa mapendekezo yake mwaka 2008 na kushauri watu wasitumie kahawa ili kujikinga na madhara ya moyo. Utafiti wa sasa ni mkubwa sana na wenye ushahidi wa kisayansi usio na shaka kiasi kwamba imebidi mamlaka husika nchini Marekani mwaka huu warekebishe mapendekezo yake ya lishe na kusema watu wasiogope tena kunywa kahawa. Taarifa hii yenye ushauri mpya imechapishwa mwezi Februari mwaka huu.

Suala la kahawa limewachanganya sana wataalamu wa afya kwa sababu tafiti nyingi zilizofanyika hapo awali zilikuwa na matokea yenye kuchanganya. Nyingine zilionesha madhara ya kahawa na nyingine faida za kahawa. Katika taaluma ya utafiti, kuna utaalamu wa jinsi ya kuchanganya matokeo ya tafiti zote nzuri na kupata matokeo ya ujumla wake (utaalamu huo unaitwa meta-analysis). Hivyo ndivyo walivyofanya akina Mostofsky na wenzake mwaka 2012 Hawa watafiti baada ya kukusanya data zote kwa pamoja, (utafiti uliohusisha zaidi ya watu laki moja na arobaini) waligundua uhusiano kati ya kahawa na magonjwa ya moyo unapochorwa katika grafu unaleta uhusiano usio katika mstari ilionyooka, bali unakuwa wa umbo kama la herufi 'J' fulani. 

Hii ilimaanisha kwamba, jinsi unavyokunywa vikombe vya kahawa, unapata faida ya kupunguza magonjwa ya moyo. Faida hiyo inaongezeka na kuwa ya juu kabisa pale unapukunywa vikombe 4 kwa siku na unapozidisha vikombe 4 faida hiyo inaanza kushuka. Kwa wale wanaokunywa vikombe 10 kwa siku na zaidi, basi hawapati faida tena bali hasara maana uwezekano wa kupata magonjwa ya moyo unaanza kuongezeka.

Utafiti huu mpya wa Choi na wenzake uliofanyika mwaka huu umetoa majibu yanayokubaliana na utafiti wa akina Mostofsky na wenzake wa mwaka 2012. Ushauri wao ni kwamba watu wanywe kahawa kwa furaha ila wasizidishe vikombe 4 au 5 kwa siku.

Matokeo ya utafiti huu yanaleta habari njema sana, kwanza kwa wanywaji wa kahawa ambao kwa muda mrefu walidhani wanadhurika kwa kunywa kahawa; pili furaha kubwa inakuja kwa wakulima wa kahawa nchini maana watajua kwamba zao la kahawa wanalojishughulisha nalo sio tu linawapa mapato bali pia linaleta faida mwilini. Habari hii njema itawatia moyo waendelee kulima kahawa kwa wingi na ubora zaidi maana kinywaji hiki kitaendelea kuhitajika sana duniani.

Pamoja na habari hizo njema zitokanazo na utafiti huu, angalizo mbili zinatakiwa kuzingatiwa: kwanza, inabidi wanywaji kahawa wasizidishe kiwango kilichoshauriwa na wanasayansi. Pili, pamoja na kwamba utafiti umeonesha kahawa inaweza kukinga magonjwa ya moyo, haimaanishi kwamba kahawa ni dawa ya kuponya magonjwa hayo. Kwa hiyo wale ambao tayari wana magonjwa ya moyo, inabidi wafuate ushauri wa madaktari wao na wasiache kuzingatia kumeza dawa zao na kufuata maelekezo mengine waliyopewa.

Mwishoni tunawashauri wataalamu wa afya wasome utafiti huu mpya kwa undani ili waweze kutoa maelezo sahihi kwa wananchi ili kuondoa hofu zisiyo za msingi kisayansi.

Unaweza kupata undani wa utafiti huu mpya kuhusu kahawa kwa kusoma machapisho tuliyoorodhesha hapa chini.
Waandishi wa makala hii ni:

Dkt Mwidimi Ndosi ni Mtafiti wa huduma za afya na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha UWE Bristol Uingereza.

Bw Mathew Mndeme ni mtafiti wa shahada ya uzamivu wa mifumo ya TEHAMA katika huduma za afya, katika Chuo Kikuu cha Leeds Uingereza, na pia ni Mwalimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

mmmwalimu(at)gmail.com

No comments:

Post a Comment