Pages

Tuesday, July 25, 2017

Wanafunzi wanaoomba kujiunga na vyuo vikuu: Je, ukasome shahada na chuo gani?

Vyuo vikuu vya Tanzania vimefungua madirisha ya usajili mpya kwa ajili ya muhula wa masomo wa mwaka 2017/2018. Sio vyuo vya Tanzania tu bali karibu nchi nyingi huu ndio muhua wa kudahili wanafunzi wapya. Hiki ni kipindi muhum sana kwa vijana wetu hasa wanaoanza shahada ya kwanza kwani ile ndoto yao ya kupata “DEGREE” na kuwa “MSOMI” ndio inaanza kuwa na ukweli. Hivyo ni muhim sana vijana hawa wakapata mwangaza wa kutosha wanapochagua chuo gani cha kujiunga na kwa ajili ya kusoma programme gani.

upload_2017-7-25_11-57-24.png 

Wale walio kwenye vyuo vikuu wanaelewa changamoto ambazo huwa tunakutana nazo kama waalimu/wahadhiri nyakati kama hizi. Wanafunzi wengi hawajui wakasome programme gani na kwa nini. Hili tatizo sio dogo kwani mara nyingine tunafundisha wanafunzi madarasani ambao hawajui walichochagua kusoma kinawapeleka wapi. Wengi hawajui nini iwe msingi wa maamuzi ya chuo gani cha kusoma. Mbaya zaidi, mara nyingi vijana hawa wanashauriana wao kwa wao au kushauriwa na watu wasio na uelewa wa mambo ya kitaalamu kwa taarifa zisizokua sahihi, zisizokua na ukweli, na za kupotoshana. Wako vijana wengi wamefeli chuo kikuu sio kwa sababu hawana uwezo bali kwa kuwa walijipachika kusoma vitu ambavyo havimo ndani yao bali walijiunga kwa mkombo, kutokujua au kushauriwa vibaya.